Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania- TPA imekabidhi vifaa Tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 30 kwa Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara -Ligula.
Vifaa Tiba hivyo vikiwemo Vitanda vya kujifungulia ( Delivery Beds) 15 vimekabidhiwa leo tarehe 09 Septemba,2023 na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mha. Juma Kijavara kwa Niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw. Plasduce Mkeli Mbossa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Ahmed Abbas ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 18 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania – TPA.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tunakuahidi sisi kama wana TPA tutaendelea kuunga mkono juhudi zako kama unavyotuunga mkono kwenye shughuli zetu za kila siku na tutakuwa bega kwa bega na wewe.” Amesema Mha. Kijavara
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Ahmed Abbas ameipongeza TPA kwa kurejesha kwa Jamii faida wanayopata na kutoa vifaa tiba hivyo kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara- Ligula.
Aidha Mhe. Kanali Abbas ameipongeza Bandari ya Mtwara kwa kupiga hatua kubwa katika kuhudumia Shehena ya mzigo mbalimbali.
“ Bandari ya Mtwara imepiga hatua kubwa katika kuhudumia Shehena ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia 2022-2023 imehudumia Shehena zaidi ya Tani Milioni 1.6 na kuvuka lengo la
Kuhudumia Shehena Tani Laki nne walilokuwa wamejiwekea.” Amesema Kanali Abbas
Akitoa neno la shukurani baada ya kupokea Vifaa tiba hivyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara- Ligula Dkt. Lobikieki Kisambu, ameushukuru uongozi wa TPA kwa msaada huo ambao unakwenda kuboresha huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali hiyo.