Baadhi ya wanafunzi wa chuo cha Kilimo Kiuma kilichoanzishwa na Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi wilayani Tunduru wakichuma pililipi Hoho kwenye shamba la mafunzo kwa vitendo.
Askofu wa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi Noel Mbawala akizungumzia juu ya kuanzishwa kwa chuo cha kilimo-Kiuma.
Sehemu ya kitalu nyumba kwa ajili ya kuotesha miche ya zao la nyanya na mazao mengine yanayotumika kwa ajili ya mafunzo kwa wanafunzi wa chuo cha kilimo Kiuma wilayani Tunduru.
Baadhi ya wanafunzi wa chuo cha Kilimo Kiuma kinachomilikiwa na kanisa la Upendo wa Kristo Masihi,wakimsikiliza Mkuu wa chuo hicho Fulko Hyera jana.
Na Muhidin Amri,Tunduru
KANISA la Upendo wa Kristo Masihi lililopo kijiji cha Milonde wilayani Tunduru,limeanzisha chuo cha masuala ya kilimo na ufugaji ili kuwapatia vijana wa mikoa ya kusini na Watanzania kwa ujumla ujuzi ambao utawawezesha kufanya kazi za kujiongezea vipato kutokana na mazao watakayozalisha.
Katibu mkuu wa Taasisi ya Kiuma Daniel Malukuta alisema,mwaka 2022 Kanisa liliona ipo haja ya kuanzisha chuo cha kilimo baada ya kubaini vijana wengi wa wilaya ya Tunduru wanakosa fursa kutokana na vigezo vya udahili wa wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na vyuo vya kilimo hapa nchini.
Alisema katika awamu ya kwanza wameanza na wanafunzi 40,ambao wanafundishwa kulima mboga mboga na matunda na hivi karibuni wataanza kozi ya ufugaji wa ng’ombe,mbuzi,kuku na samaki.
Alisema,kuanzishwa kwa chuo hicho ni sehemu ya mchango wa taasisi ya Kiuma kwa jamii ya wananchi hasa wanaoishi katika mikoa ya kusini ambao bado wako nyuma kimaendeleo licha ya mikoa hiyo kuwa na rasimili nyingi.
“hapa tunamfundisha mtu kulima na kuzalisha iwe mazao ya kilimo au mifugo,tumeanza kulima matunda na mboga mboga na baada ya muda mfupi tutaanza kufundisha kozi ya ufugaji wa kuku,mbuzi,ng’ombe na samaki”alisema.
“malengo yetu ni kuendelea kuwagusa watanzania wa maeneo ya kusini ambao bado fursa nyingi zinawapita na maisha yao bado yako chini licha ya mikoa hiyo kuwa na rasilimali nyingi ambazo bado hazijatumika ”alisema Malukuta.
Aliongeza kuwa,huo ni mchango mkubwa na wataendelea kushirikiana na serikali ya awamu ya sita katika kuwasaidia wanyonge,kujiunga na chuo hicho kilichoanzishwa kwa ajili ya watu wote.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Noel Mbawala alisema,chuo hicho kitakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa mikoa ya kusini ambao kwa muda mrefu walibaki nyuma kielimu na maendeleo.
Alisema,chuo ni kikubwa na kimeanza kufanya vizuri kwa kuwafundisha vijana juu ya kilimo cha kisasa kwa kutumia mbolea za asili na vijana waliojiunga na chuo hicho mbali na kupata elimu ya kilimo cha kisasa,lakini watapata ujuzi wa kutengeneza mbolea za asili.
Alisema,malengo makubwa ya kanisa kupitia taasisi ya Kiuma ni kuwafikia Watanzania wote bila kujali tofauti za dini,kabila ili waweze kunufaika na huduma zinazotolewa na taasisi hiyo ikiwemo huduma za kiroho,afya,elimu na ufundi na kuisaidia serikali kumaliza tatizo la ajira.
Aidha alisema, katika kufanikisha mpango huo wamekuwa na utaratibu wa kutoa ajira kwa baadhi ya vijana wanaomaliza kwenye vyuo vinavyomilikiwa na Kiuma kama vile chuo cha ufundi,ukunga na utabibu baada ya kuhitimu mafunzo yao.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho Fulko Hyera alisema,malengo makubwa ya chuo kusaidia jamii hasa vijana walioko mtaani ambao wamemaliza elimu ya kidato cha nne na sita lakini wako mtaani kwa sababu mbalimbali.
“tumeona ni bora hawa vijana tuwachukue tuwaweka hapa ili tuwape mafunzo na kuwajengea uwezo wa kuzalisha mazao ambayo hapo baadaye yatawasaidia kufanya biashara,kuwapa ujuzi wa kufuga ili kuwapatia kipato kutokana na mahitaji ya uko mtaani”alisema.
Aidha amelitaja kundi lingine lililokusudiwa katika mpango huo ni vijana waliomaliza vyuo vya ualimu na vyuo vikuu lakini wamekosa fursa ya kuajiriwa serikali,lakini kupitia mafunzo hayo wataweza kujiajiri na wengine kufanya biashara za mazao ya kilimo.
“tunapozungumzia kilimo hasa katika mikoa ya kusini vijana wengi wanaona kama ni adhabu,kwa hiyo sisi tunayofanya ni kuwaandaa kisaikolojia kuwa wajasiriamali,tunawapatia mbinu na kuwajengea uwezo ili baadaye waweze kuzalisha kwa wingi kwa kuwa kilimo ni mtaji,kilimo ni biashara,ni kazi kama nyingine”anasema Hyera.
Alisema,chuo kinatoa mafunzo kwa miaka mwili na katika mwaka wa kwanza wanajifunza zaidi kilimo cha mboga mboga ambacho wanaangalia mahitaji ya jamii ya kila siku hasa mboga mboga ambazo zinazosaidia kuongeza lishe na kuongeza virutubisho kwenye mwili wa binadamu.
Ametaja mboga mboga zinazozalishwa katika shamba la kujifunzia ni kabichi,nyanya,pilipili,bilinganya,nyanya,karoti,vitunguu,bamia ambapo wanatoa mafunzo ya nadharia darasani na vitendo.
Anasema katika hatua ya kwanza, vijana wanafundishwa namna ya kuandaa shamba,matuta na vitalu nyumba(green House) na kupitia njia hiyo mkulima anatumia eneo dogo la uzalishaji lakini akilihudumia vizuri atapata mazao na mapato mengi.
Anasema,hatua ya pili wanafundishwa kutengeneza mbolea ya mboji(asili) ambayo inatengenezwa kwa kutumia mabaki ya mimea,nyasi,mashudu ya alizeti na samadi inayochanganywa na udongo.
Anaeleza kuwa,mbolea ya asili ina faida nyingi kwenye uzalishaji ikiwemo kumpunguzia mkulima gharama ambayo upatikanaji wake unahitaji fedha nyingi na kusababisha baadhi ya wakulima kushindwa kumudu gharama.
Mmoja wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo hicho Asinath Juma,anaiomba serikali kuwasaidia juu ya suala la mikopo kwa vijana wanaotoka katika vyuo vya kilimo ili waweze kupata mitaji na kuendeleza ujuzi waliopata kupitia vyuo vya kilimo.
Alisema,hatua hiyo itawasaidia vijana wengi wanaomaliza kwenye vyuo hivyo kuwa mfano bora kwa jamii kwa kuzalisha na kufungua mashamba ambayo yatatumika kama mashamba darasa kwa watu wanaowazunguka uko waendako.