Na. WAF Dodoma
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amesema katika kuendeleza mikakati ya kutoa chanjo dhidi ya Polio, wizara imeunda timu ya watoa huduma 5,291 waliopata mafunzo ya kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio katika Mikoa sita nyumba kwa nyumba .
Prof. Nagu ameyasema hayo katika kikao cha waziri wa afya na waandishi wa Habari leo Jijini Dodoma akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio ambayo inatarajiwa kuanza kufanyika nchini kuanzia Septemba 21 hadi 24, 2023.
“Wakati wa Kampeni kutakuwa na jumla ya timu yenye jumla ya watoa huduma za afya 5,291 kwa Mikoa sita (6) itakayofikiwa na zoezi hili ambapo kila timu itakuwa na watoa huduma watatu. Timu hizi zitakuwa zinatoa huduma ya chanjo kwa walengwa kupitia vituo vya kutolea huduma za afya, nyumba kwa nyumba, shuleni na maeneo mbalimbali ya mikusanyiko ikiwemo Nyumba za Ibada”.
Pia Prof. Nagu amesema wizara imeumeunda timu nzuri ambayo imepata mafunzo ya kutoa chanjo ili kuhakikisha watoto wote wanafikiwa katika kupatiwa Chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio” amesema Prof. Nagu.
Aidha Prof. Nagu ametoa rai kwa wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa watoa huduma za afya ili kuwezesha watoto wao kuchanjwa kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba.”
“Tunawapa hamasa wazazi wahakikishe kwamba, wanawatoa watoto wao kupata chanjo hii ili kuwaepusha watoto wetu kupata ulemavu ambao kwakweli unakingika kwa kutumia chanjo”. Ameongezea Prof. Nagu.