Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema Tanzania Ina mengi ya kujifunza kutoka nchini Algeria katika Sekta ya Michezo kutokana na nchi hiyo kupiga hatua kubwa katika eneo hilo.
Katibu Mkuu Yakubu amebainisha hayo hivi karibuni alipofanya mazungumzo na Bw. Lahcen Ladjadj Mkurugenzi wa Michezo na Vijana wa Jiji la Constantine, Algeria, ambapo alielezwa kuwa nchi hiyo ina Vyuo Vikuu 20 maalum kwa ajili ya michezo, viwanja vingi vyenye hadhi na ukubwa unaotambulika na FIFA pamoja na programu za kubaini na kukuza vipaji vya michezo kwa watoto.
Katika Mazungumzo yao, Mkurugenzi huyo amesema Jiji hilo litashirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutoa mafunzo, ambapo pia ametoa mwaliko rasmi kwa viongozi hao kutembelea Jiji hilo ili kuona na kujifunza uwekezaji wa miondombinu ya michezo katika Jiji hilo kutokana na historia na uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Algeria.
Jiji hilo ndio lilikua kambi ya wiki moja ya maandalizi ya Timu ya Taifa ya Algeria kabla ya mchezo wake na Taifa Stars uliochezwa jana ambao ulimalizika kwa sare ya bila kufungana na timu hizo kufuzu mashindano ya AFCON 2023 nchini Ivory Coast.