Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu utoaji wa chanjo ya matone ya Polio awamu ya pili katika mikoa sita Tanzania bara.
Na.Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI inatarajia kuendesha kampeni maalum ya siku ya nne ya utoaji wa chanjo ya matone ya Polio awamu ya pili katika mikoa 6 Tanzania Bara lengo likiwa ni kuwafikia watoto Milioni 3.2 walio chini ya umri wa miaka 8.
Kampeni hiyo inayoanza Septemba 21 hadi 24 mwaka huu, inafanyika kutokana na nchi tunazopakana nazo kama Burundi,Zambia na Demokrasia ya Congo kuwa na maambukizi lakini pia hapa nchini mwezi Mei 2023 ilipata taarifa ya uwepo wa mtoto wa Mwaka mmoja katika Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa aliyegundulika kuwa na maambukizi ya Virusi vya Polio.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametoa taarifa hiyo leo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema mikoa ambayo inapakana na nchi zenye mlipuko wa polio ambayo ni Rukwa, Kagera, Kigoma, Mbeya, Katavi na Songwe.
Aidha ameitaja idadi ya watoto wanaotarajiwa kufikiwa na chanjo hiyo kwenye mabano ni Mkoa wa Rukwa(391,883), Kagera (729,387), Kigoma (884,477), Mbeya (614,346), Katavi (227,862) na Songwe 402,643.
“Ili kutekeleza kampeni hii niwaelekeze Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya katika mikoa hiyo sita kusimamia kwa karibu maandalizi na utoaji wa chanjo katika kampeni hii,waganga wakuu wa mikoa na halmashauri wahakikishe chanjo zinakuwepo za kutosha na Mganga Mkuu wa Serikali ahakikishe elimu inafika kwa wananchi,”amesema Waziri Ummy
Hata hivyo Waziri Ummy ametoa rai kwa wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa watoa huduma za afya ili kuwezesha watoto wao kuchanjwa kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba.
Mara ya mwisho Tanzania kugundulika kuwa na Polio ni mwaka 1996 ambapo mwaka 2015 Shirika la Afya Duniani (WHO),iliitangaza Tanzania kuwa ni nchi iliyotokomeza ugonjwa wa Polio.