Mkurugenzi wa shule ya mchepuo wa kiingereza ya Bethlehem Star Pre &Primary iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha,Edgar Walter akizungumza katika mahafali hayo jijini Arusha .
Julieth Laizer ,Arusha .
Serikali imeombwa kufuatilia na kudhibiti wizi wa mitihani unaofanywa katika shule mbalimbali ili watoto waweze kujifunza maadili mema wakiwa tangu wadogo na kuweza kupata viongozi wa baadaye walio bora na waadilifu.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkurugenzi wa shule ya mchepuo wa kiingereza ya Bethlehem Star Pre &Primary iliyopo wilayani Arumeru mkoani Arusha,Edgar Walter wakati akizungumza na wanafunzi na wazazi katika mahafali ya 4 ya darasa la saba ambapo jumla ya wanafunzi 28 walihitimu.
Amesema kuwa, kitendo kinachofanywa na baadhi ya shule cha wizi wa mitihani kinawajengea watoto sifa mbaya kwani kinawafanya washindwe kutumia akili zao wenyewe na hivyo kuwajengea dhana ya kutokuwa waaminifu.
“Naiomba serikali itusaidie kudhibiti swala hilo la wizi ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya shule kwa lengo la kuwezesha watoto wao wafaulu kwani jambo hilo haliwajengi watoto katika misingi iliyo bora kwa manufaa yao ya baadaye.
Aidha amesema kuwa, shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba kutokana na maandalizi mazuri ambayo wamekuwa wakiandaliwa na walimu shuleni hapo.
Aidha akizungumzia changamoto inayowakabili shuleni hapo amesema kuwa ni ubovu wa barabara kutoka Roterdam hadi kufikia shule ya Muungano hali ambayo inawasababisha magari kushindwa kufika shuleni kwa wakati hasa kipindi cha masika, kwani imekuwa ni changamoto kubwa sana kwao,hivyo aliomba serikali kuwasaidia kushughulikia changamoto hiyo ya muda mrefu.
Aidha amewataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri katika kuiwakilisha shule hiyo kwa kufanya vizuri katika masomo yao huku waondokana na makundi mabovu yasiyofaa ambayo yatawaharibia maisha yao ya baadaye.
“Nitumie nafasi hii pia kuwataka wazazi pamoja na walezi kutoa motisha kwa watoto wao ili kuongeza hari zaidi katika masomo yao na kuweza kuendelea kwani hapo bado kabisa ndo wameanza .”amesema .
Kwa upande wake mgenirasmi katika mahafali hayo Afisa tarafa ya Poli,Said Mzava aliyemwakilisha Mkuu wa wilaya ya Arumeru ,amewataka wahitimu hao kutuliza akili wakati wakiwa kwenye chumba cha mitihani kwani mtihani ni wa kawaida tu na ilivyo mitihani mingine huku akiwataka kuvunja rekodi na kuiwakilisha vyema wilaya huyo kwa kuwa kinara wa shule zinazoongoza.
“Mimi nawaomba wazazi kuhakikisha wanatoa motisha kwa watoto wao na kuwatia moto ili wawe na moyo wa kusoma zaidi na kuweza kufikia malengo yao waliyojiwekea. “amesema.
Kwa upande wa Mkuu wa shule hiyo Anosisye Kapushi ,amesema kuwa shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri sana katika matokeo ya darasa la saba mfululizo kutokana na jinsi wanavyoandaliwa na walimu wao na kuweza kufanya vizuri zaidi katika mitihani yao.
Amesema kuwa ,shule hiyo ilianzishwa mwaka 2017 ambapo ina jumla ya wanafunzi 303 ambapo wamekuwa wakifundisha somo la kompyuta kwa kuanzia madarasa ya awali ili kuwawezesha watoto hao kulijua somo hilo mapema wakiwa bado wadogo.