MBUNGE wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu amehoji serikali mpango wa kujenga nyumba za askari polisi ikiwamo Wilaya ya Ikungi kutokana na wengi wao kulazimika kupanga nyumba mitaani.
Akiuliza maswali Bungeni Septemba Mosi,Mwaka huu Mtaturu amesema kuna uhaba mkubwa wa makazi ya askari na katika wilaya hiyo hakuna nyumba hata mmoja ya askari na hata Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya analazimika kupanga nyumba mtaani.
“Ni lini sasa Serikali itajenga vituo vya Polisi kwenye kata za Mkiwa, Misughaa na Mungaa kwenye jimbo hilo kutokana na ukuaji wa kiuchumi unaongeza matatizo ya kiusalama kwenye maeneo mbalimbali,”amehoji.
“Tulikubaliana kuwa na polisi kata sasa polisi kata bila kituo ni sawa na bure,Je nini mkakati wa serikali wa kujenga vituo hivi hasa kata za pembezoni ili kusaidia ulinzi.,kwak uwa tayari wananchi wamefyatua matofali 1,000 katika kata ya Mkiwa na kupitia mfuko wa jimbo na mimi nimeanza kuwaunga mkono, je nini serikali itafanya kusaidia kukamilisha ujenzi huu,”ameuliza Mtaturu.
Akijibu maswali hayo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema moja ya mikakati ya serikali ni kuimarisha ulinzi na usalama kwa kuhakikisha askari wanaishi maeneo stahiki karibu na maeneo ya kazi na kupitia bajeti zake itaendelea kutenga fedha kwa ajili hiyo.
“Serikali inazo taarifa kuwa Kata za Mkiwa, Misughaa na Mungaa zimeshatenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Polisi na nyumba za makazi ya askari,na serikali kupitia Jeshi la Polisi inasubiri kupata taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa vituo na nyumba hizo ili kuunga mkono kwenye ukamilishaji,”amesema.