Wanafunzi kutoka shule hizo mbili wakiwa na walimu wakikabithiwa meza kwa ajili ya shule hizo zilizopo halmashauri ya Meru mkoani Arusha
Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya Meru ,Felister Nanyaro akizungumza katika halfa hiyo jijini Arusha leo .
Mratibu mkazi kutoka shirika la TES School in Africa hapa Tanzania,Steven Ndosi akizungumza katika hafla hiyo ya kukabithi Samani hizo jijini Arusha.
Wanafunzi kutoka shule hizo mbili wakiwa na walimu wakikabithiwa meza kwa ajili ya shule hizo zilizopo halmashauri ya Meru mkoani Arusha
Wanafunzi kutoka shule hizo wakiwa wameshika kiti baada ya kukabithiwa rasmi na Shirika la TES School in Africa .
Julieth Laizer ,Arusha .
Wanafunzi wa shule ya msingi Ambureni na Nkoanrua halmashauri ya wilaya ya Meru mkoani Arusha wameondokana na changamoto ya kusongamana darasani kutokana na uhaba wa Samani, baada ya kupatiwa msaada wa viti na meza kutoka shirika la TES School in Africa kutoka nchini Denmark.
Akizungumza katika hafla ya kukabithi Samani hizo kwa shule hizo, Mratibu mkazi wa shirika hilo la TES School in Africa hapa Tanzania ,Steven Ndosi amesema kuwa, shirika hilo lilianzishwa mwaka 2014 huko Denmark ambapo linajishughulisha na kutafuta marafiki wafadhili wa shule za msingi na sekondari ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa walimu na wanafunzi .
Aidha amesema kuwa, lengo la kusaidia shule hizo ni ili kuinua kiwango cha elimu mashuleni na kuweza kuwasaidia wanafunzi hao kusoma katika mazingira mazuri sambamba na kuondoa msongamano madarasani kutokana na uhaba wa meza na viti.
Ndosi amesema kuwa, kwa mwaka jana walitoa msaada wa jiko la kisasa la kupikia kwa shule ya sekondari Poli,huku wakiweka umeme wa jua kwa shule za msingi Ambureni na Moivaro ,pamoja na kukabithi Samani za kisasa kwa shule ya sekondari Poli na shule za msingi za Ambureni na Moivaro.
Aidha amesema kuwa,lengo la shirika hilo ni kufikia shule nyingi kadri iwezekanavyo ili kupunguza ama kuondoa kabisa changamoto ya Samani katika shule za msingi na sekondari katika halmashauri ya wilaya ya Meru.
“Leo tumekabithi madawati na meza pamoja na viti na mbao za kisasa za kuandikia darasani na vifaa vingine vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shs 70 milioni vifaa ambavyo vitaweza kutumiwa na wanafunzi 370 kwa shule za msingi Ambureni na Nkoanrua. “amesema Ndosi.
Aidha ameongeza kuwa, kwa mwaka huu 2024 wanatarajia kuleta Samani, kompyuta na LCD Projector kwa ajili ya shule ya sekondari Nkoanrua na Naurey Golden Soils ambapo wameweza kufanya mazungumzo na shule ya sekondari Amsha kijiji cha Moivaro halmashauri ya Meru na kuwa watawaletea vifaa vya ufundishaji na ujifunzaji kama walivyofanya kwa shule zingine.
Aidha amesema katika mchakato wa kuleta kontena hilo wamekabiliwa na changamoto ya uwepo wa urasimu katika upatikanaji wa nyaraka mbalimbali kama msamaha wa kodi na upatikanaji wa fedha za kulipia ongezeko la thamani kwani changamoto hizo zimesababisha usumbufu mkubwa kiasi ambacho kontena lilichelewa kuondolewa bandarini ambapo ucheleweshaji huo ulipelekea kupigwa faini ya 1,080,000 jambo ambalo ni changamoto na linawakatisha tamaa wafadhali wanaotusaidia.
Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya Meru ,Felister Nanyaro akizungumza katika halfa hiyo alipongeza shirika hilo kwa namna ambavyo wanaunga mkono serikali katika swala la elimu ambapo aliwaomba kuangalia namna ya kuzisaidia shule zilizopo pembezoni kwani zinakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Alitumia fursa hiyo kuwataka wazazi pamoja na walezi kuzungumza na watoto wao kuhusiana na maswala ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ndoa za jinsia moja unaoendelea kwenye jamii ili nao waweze kukemea vitendo hivyo.
Nao baadhi ya wanafunzi wa shule zilizonufaika,walishukuru kwa msaada huo kwani inawaondolea changamoto ya kusongamana darasani kwani katika kiti kimoja badala ya kukaa watatu sasa hivi watakaa wawili na kuwaongezea umakini katika masomo yao.