Ndugu wanahabari,
- Nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Mataifa, ikiwemo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zimesaini na kuridhia mikataba, Itifaki, maazimio na makubaliano mbalimbali ya Kuzuia Uzagaaji wa Silaha Ndogo na Nyepesi. Moja ya makubaliano hayo ni makubaliano ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika mwezi Julai 2018 kuhusu udhibiti wa uzagaaji wa silaha haramu. Uzagaaji wa silaha haramu duniani umekuwa ukisababisha uvunjifu wa amani, ukosefu wa usalama na kusababisha hofu kwa watu, vifo na majeruhi.
- Aidha, hata kabla ya maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya mwaka 2018, Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika tayari zilikuwa zimefikia maazimio juu ya udhibiti wa silaha haramu katika Mkutano wa Wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika uliofanyika kuanzia tarehe 03 – 04 Julai, 2017 Jijini Addis Ababa – Ethiopia ambapo iliazimiwa kuutangaza mwezi Septemba kila mwaka kuwa ni mwezi wa usalimishaji wa silaha haramu kwa hiari sambamba na kutoa msamaha kwa wahusika kutoshitakiwa endapo watasalimisha silaha hizo haramu kwa hiari na kwa muda uliopangwa.
- Hivyo, kwa kuzingatia msingi wa maazimio ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa
Afrika na kwa mamlaka niliyopewa chini ya Kifungu cha 64 cha Sheria ya Udhibiti wa Silaha na Risasi ya Mwaka 2015, Sura ya 223, nawatangazia Msamaha wa kutoshitakiwa watu wote wanaomiliki silaha kinyume cha Sheria kupitia Tangazo la Serikali Na. 619 la tarehe 25/8/2023 endapo watasalimisha silaha hizo kwa kuzingatia masharti yafuatayo:–
- i.
Usalimishaji wa silaha haramu kwa hiari nchi nzima utafanyika kuanzia tarehe 01/9/2023 hadi 31/10/2023.
- ii. Silaha haramu zitapaswa kusalimishwa katika kituo chochote cha Polisi nchini, Ofisi ya Serikali za Mitaa au kwa Mtendaji Kata/ Shehia kuanzia muda wa saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni.
- Mtu yeyote atakayesalimisha silaha haramu nje ya muda ulioainishwa katika
tangazo la Msamaha atachukuliwa hatua za kisheria.
- Mwaka jana mwezi Septemba, 2022 Serikali ilitoa msamaha wa kutoshitakiwa, ikiwataka wale wote wanaomiliki silaha kinyume na Sheria kuzisalimisha kwa hiari. Hata hivyo baadhi ya wananchi hawakuitikia wito huo. Jeshi la Polisi kupitia operesheni mbalimbali liliweza kuwakamata na kuwafikisha mahakamani jumla ya watuhumiwa 221 kwa kosa la kumiliki silaha Kinyume na Sheria na watuhumiwa 17 kwa kosa la kumiliki risasi kinyume na Sheria.
- Hivyo natoa wito kwa wananchi wote wanaomiliki silaha kinyume na Sheria kuhakikisha kuwa wanatumia fursa hii adimu ili kuepuka kukumbwa na mkondo wa sheria kwa kuwa baada ya kipindi cha msamaha kuisha, Jeshi la Polisi litaendesha msako nchi nzima ili kuwabaini na kuwakamata wale wote watakaopatikana wakimiliki silaha kinyume cha Sheria.
- Vilevile, nachukua fursa hii kuwasisitiza wananchi wote ambao ndugu zao walikuwa wanamiliki silaha kihalali na sasa wamefariki kuhakikisha wanazisalimisha silaha hizo kulingana na masharti niliyoyataja.
- Aidha, nawaasa wamiliki wote wa silaha kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya matumizi mabaya na utunzaji mbaya wa silaha huku mkizingatia Sheria na Kanuni. Na yeyote atakayekiuka Sheria na Kanuni husika, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kufutiwa Leseni.
- Niwaombe Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ambao kimsingi
ni Wenyeviti wa Kamati za Usalama kuratibu zoezi hili kwa ukamilifu.
- Pia niwaombe Viongozi wa Serikali za Mitaa na Watendaji wa Kata kutengeneza mazingira ya kuwapokea wananchi wote watakaosalimisha silaha kwa hiari na kutoa taarifa katika vituo vya Polisi vilivyo karibu.
- Aidha, nalielekeza Jeshi la Polisi kuandaa mpangokazi wa kila siku wa kukusanya silaha zitakazosalimishwa katika Ofisi za Serikali za Mitaa na katika Ofisi za Watendaji wa Kata na kutoa taarifa ya ujumla mara zoezi hili litakapokamilika.
Hamad M.Y Masauni (Mb)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI
30 AGOSTI, 2023