Makamu wa Rais Mstaafu na Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Dkt. Mohamed Gharib Bilal akiongea wakati wa hafla ya kuwasimika Mkuu wa taasisi Bw. Omari Issa na Makamu Mkuu wa taasisi , Profesa Maulilio Kipanyula.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia, anayeshughulikia masuala ya Sayansi Profesa James Mdoe akizungumza na Watumishi wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia pamoja na wageni waalikwa wakati wa Hafla ya Kuwasimika Mkuu wa Taasisi na Makamu Mkuu wa taasisi.
Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Bw. Omari Issa akitoa neno la shukrani wakati wa hafla ya kusimika viongozi wa Taasisi hiyo Agosti 30,2023.
Makamu wa Rais Mstaafu na Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Dkt. Mohamed Gharib Bilal (kulia) akimsimika Mkuu wa Taasisi Bw. Omari Issa (Katikati) Agosti 30,2023, Kushtoto ni Mkuu wa Ndaki Sayansi ya Viumbe Hai na Bailojia Professa Ernest Mbega.
Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Bw. Omari Issa (Kushoto) akimsimika Makamu Mkuu wa Taasisi Prof. Maulilio Kipanyula (katikati) , kulia ni Mkurugenzi wa Taaluma Dkt. Efraim Kosia.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia, anayeshughulikia masuala ya Sayansi Profesa James Mdoe (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya Taasisi wakati wa Hafla ya Kuwasimika Mkuu wa Taasisi na Makamu Mkuu wa taasisi Agosti 30,2023.
Na Mwandishi Wetu, Arusha
Makamu wa Rais Mstaafu na Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Dkt. Mohamed Gharib Bilal ameitaka Taasisi hiyo kuzidi kung’ara katika masuala ya tafiti na bunifu kwa maendeleo ya nchi na Afrika kwa ujumla.
Dkt. Bilal ameyasema hayo Agosti 30, 2023 wakati wa hafla ya kumsimika Mkuu wa taasisi hiyo mpya Bw. Omari Issa sanjari na kumsimika Makamu Mkuu wa taasisi , Profesa Maulilio Kipanyula.
“Ninahamu ya kuona taasisi hii inapiga hatua zaidi na najua mwenzangu Bw. Omari Issa ataiweka taasisi hii katika anga za juu zaidi” alisema Dkt. Bilal
Aliongeza kuwa taasisi ya Nelson Mandela ni imara na ya kipekee nchini hivyo anatamani kuiona ikipaa zaidi katika anga za juu katika tafiti , bunifu na teknolojia huku akiwapongeza watumishi wa taasisi hiyo kwa kuhakikisha jina la NM-AIST linapaa zaidi.
Naye Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia, anayeshughulikia masuala ya Sayansi Profesa James Mdoe ameeleza kuwa wizara ina matarajio makubwa kupitia uongozi huo mpya ikiwemo kuongeza mchango wa sayansi na teknolojia katika kuchagiza maendeleo ya nchi.
“Mmemsikia Mkuu wa chuo anataka ongezeko la wanawake chuoni hapa ili kupata wanataaluma wengi zaidi katika sayansi na teknolojia “Alisema Naibu Katibu Mkuu Professa James Mdoe
Professa Mdoe anaeleza kuwa kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEETProject) Wizara kupitia Vyuo Vikuu inatarajia kuanzisha kozi maalum ili kuwasaidia wanawake wasiofikia ufaulu waweze kupata ufaulu na kuruhusu kujiunga na vyuo vikuu ili kuongeza msukumo kwa wanawake na wasichana kujiunga na vyuo vya Sayansi na Teknolojia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi Bw. Omari Issa anaeleza kuwa uongozi wa Dk. Bilal umefanikiwa katika mambo mbalimbali ikiwemo ongezeko la udahili wa wanafunzi kutoka wanafunzi 80 hadi kufikia wanafunzi 1,468 na ujenzi wa Bweni linaloendelea kujengwa ambalo linauwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 500 na vyumba maalum kwa ajili ya wanafunzi wakike wanaonyonyesha na wajawazito.
“Naomba nisisitiza udahili wa wanafunzi wa kike lazima uongezeke zaidi kwani wanawake wanaweza zaidi katika nyanja za kila aina hivyo katika kipindi cha uongozi wangu udahili wa wanawake uzingatiwe”. Bw. Omari Issa
Hafla hiyo ya kusimikwa kwa Wakuu wa Taasisi umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mwakilisha wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambaye ni Afisa Elimu Taaluma Mkoa Bw. Emmanuel Mahundo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia upande wa Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe na Mwenyekitiwa Baraza la Chuo na Mkuu wa Chuo cha Dodoma Professa Lughano Kusiluka.