Matenki ya kuhifadhia maji yanayotumika kwenye mradi wa maji Kitai wilayani Mbinga ambao ukikamilika utamaliza changamoto ya maji katika gereza la Kitai na kitongoji cha Ngembambili.
Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira(Ruwasa)Mhandisi Lucy Koya, akikagua baadhi ya miundombinu kwenye mradi wa maji Kitai unaotekelezwa na Ruwasa wilayani Mbinga kwa gharama ya Sh.milioni 560.
Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira(Ruwasa)Mhandisi Lucy Koya akifungua bomba ili kuhakikisha wingi wa maji yanayoingia kwenye matenki yanayohudumia zaidi ya wakazi 1,468 wa Gereza la Kitai na kitongoji cha Ngembambli wilayani Mbinga,katikati kaimu Mkurugenzi wa Ruwasa Bwai Biseko na kulia meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbinga Mashaka Sinkala.
Kaimu Mkurugenzi wa Ruwasa Bwai Biseko kulia na Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Mhandisi Lucy Koya kushoto wakifungua koki katika moja ya vituo vya kuchotea maji vilivyojengwa katika gereza la kilimo la Kitai wilayani Mbinga baada ya kukagua utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji utakaohudumia zaidi ya wakazi 1,468,katikati Mkuu wa Gereza hilo Mrakibu wa Magereza Gabriel Rudeligo.
Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira Mhandisi Lucy Koya,akimtiwisha ndoo ya maji mkazi wa Kitai Consolatha Haule baada ya kutembelea mradi wa maji Kitai unaotekelezwa na Ruwasa kwa gharama ya Sh.milioni 560,anayeshuhudua Mkuu wa Gereza la kilimo Kitai wilayani Mbinga Gabriel Rudeligo.
Mkuu wa Gereza la kilimo Kitai wilayani Mbinga Mrakibu wa Magereza Gabriel Rudeligo kulia akitoa shukrani kwa Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Ruwasa nchini Mhandisi Lucy Koya baada ya Ruwasa kuanza ujenzi wa mradi wa maji utakaohudumia gereza hilo,wengine katika picha ni baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Kitai ambao ni miongoni mwa wanufaika wa mradi huo.
Na Muhidin Amri,
Mbinga
ZAIDI ya wakazi 1,464 wa Kitai na Ngembambili wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,wanatarajiwa kuondokana na kero ya uhaba wa maji safi na salama baada ya wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira(Ruwasa)kuanza ujenzi wa mradi mkubwa wa maji utakaogharimu zaidi ya Sh.milioni 560.
Mkuu wa Gereza la Kitai Mrakibu wa Magereza Gabriel Rudeligo alisema,kero ya maji safi na salama ni ya muda mrefu kutokana na kukosekana kwa chanzo cha uhakika hivyo kupelekea wakazi wanaoishi katika eneo hilo wakiwemo askari na familia zao kulazimika kutumia maji ya visima vya asili na mito ambayo siyo safi na salama.
Rudeligo,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutoa fedha kwa wizara ya maji na Ruwasa kuanza ujenzi wa mradi huo ambao ukikamilika utamaliza kilio cha muda mrefu cha ukosefu wa maji safi na salama iliyokuwepo tangu Uhuru.
Alisema,kila siku katika eneo la Gereza kuna mkusanyiko mkubwa wa watu hasa wafungwa,wanafunzi wa shule ya msingi,wananchi wanaofika kupata huduma za matibabu kwenye zahanati na familia za askari ambao wanahitaji huduma ya maji ya uhakika kwa ajili ya matumizi ya kila siku .
Mkuu wa Gereza alisema,ni faraja kubwa kama kiongozi wa eneo hilo kuona kilio cha maji sasa kinakwenda kumalizika na kuwapongeza wataalam wa Ruwasa wilaya ya Mbinga na mkoa kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.
Aliongeza kuwa,pindi mradi huo utakapo kamilika utawaondolea adha na kero kubwa ya kwenda kutafuta maji kwenye vyanzo vya asili ambavyo havikutosheleza mahitaji yao,hali iliyosababisha baadhi ya shughuli za uzalishaji mali kufanyika kwa kusua sua licha ya nguvu kazi kubwa waliyonayo.
Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa usambazaji maji na usafi wa mazingira(Ruwasa)Mhandisi Lucy Koya,amewataka wananchi wanaoishi katika eneo hilo na maeneo ya jirani kuhakikisha wanatunza mradi huo ili uweze kudumu kwa muda mrefu na kuwa suluhisho la changamoto ya maji kwao.
Aidha,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia fedha Ruwasa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji ikiwemo mradi wa maji Kitai ambao unakwenda kutimiza dhamira yake ya kumtua mama ndoo kichwani.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbinga Mashaka Sinkala alisema,mradi wa maji Kitai utahudumia takribani wakazi 1,468 kati yao 1,204 ni kutoka Gereza la Kitai,shule ya msingi na Zahanati na wakazi 264 kutoka Kitongoji cha Ngembambili ambacho ni maarufu kwa uchimbaji wa madini.
Alisema,mradi huo unatekelezwa kwa kutumia wataalam wa ndani na ulianza kutekelezwa mwezi Februari 2023 na ulitakiwa kukamilika mwezi Juni,lakini muda wa utekelezaji wake uliongezwa hadi mwezi Septemba kutokana na sababu za mvua kubwa zilizonyesha na mwingiliano wa kazi hususani za uchimbaji wa mitaro ambazo zilizofanywa na wafungwa wa gereza hilo.
Alitaja lengo kuu la mradi huo ni kutoa huduma ya maji kwa jamii inayoishi katika eneo na ndani ya gereza la kitai ambalo lilikuwa na uhaba mkubwa wa maji ambapo ukikamilika utasaidia sana kupunguza magonjwa ya mlipuko na kutoa fursa kwa jamii kupata muda wa kushiriki shughuli mbaimbali za kiuchumi.
Alisema,mradi huo utagharimu zaidi ya Sh.milioni 560 na hadi sasa fedha zilizotumika ni Sh.321,710,650.44 sawa na asilimia 57.4 ambazo zimetumika kwa kununua mabomba,tenki na vifaa vingine vya kujengea.
Mganga mkuu wa zahanati ya Kitai Jackson Kapinga alisema,changamoto ya maji imesababisha kuongezeka kwa wagonjwa wanaofika kutibiwa katika zahanati hiyo hasa wale wanaougua magonjwa ya Ngozi,matumbo na Typhoid.