Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi Balozi. Mha. Aisha Amour, akizungumza Leo Agosti 29,2023 Jijini Dodoma wakati akifungua Kikao Cha Tisa Cha Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB). |
Baadhi ya Washiriki wa Kikao Cha Tisa Cha Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) kilichofanyika Leo Agosti 29,2023 Jijini Dodoma. |
Na Okuly Julius-Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi Balozi. Mha. Aisha Amour amewataka wafanyakazi wa Bodi ya usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB),kufanya kazi Kwa kujituma na kuepuka Vitendo vya Rushwa.
Balozi Amour ametoa kauli hiyo Leo Agosti 29,2023 Jijini Dodoma wakati akifungua Kikao Cha Tisa Cha Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB).
“Kutokuwa na weledi na uadilifu na uwepo wa Makundi inapelekea kudorora Kwa ufanisi wa utendaji kazi baina yenu kama watumishi wa umma na nitangaze rasmi hapa hatutaweza kumvumilia mtumishi yeyote atakayekuwa kikwazo katika utendaji kazi,”amesema Balozi Amour
Katibu Mkuu huyo amesema hakutakuwepo na nafasi ya kumhamishia mtumishi wa Umma kisa ameshindikana au kashindwa kutimiza majukumu yake vyema Kwa nafasi aliyepo zaidi ni kumuondoa kwenye mfumo wa ajira ili wengine wachukue nafasi na kufanya kazi kwa weledi na uadilifu.
“Hatutampokea mtumishi aliyeota mapembe na kushindikana huko aliko kikubwa tutamuondoa kwenye mfumo ili akafanye kazi kwingine nje ya utumishi wa Umma Kwani tukikutoa huko tukakuhamishia sekta nyingine utaendeleza yaleyale,”amesisitiza Balozi Amour.
Pia amewapongeza viongozi wa Bodi hiyo Kwa kuondoa kikao hicho ambacho ndani yake kutakuwa na mada mbalimbali ikiwemo ya Maadili ya kazi na kuwataka wahakikisha watumishi wanapata Mafunzo ya mara Kwa mara ya Mahala pa kazi ili kuendelea kuwajengea uelewa na kuwakumbusha misingi ya kazi.
Aidha,Katibu Mkuu huyo ameagiza ufuatiliaji wa uwepo wa vitendo vya Rushwa baina ya wafanyakazi wa Bodi hiyo hasa pale wanapokwenda kupima na kukagua Majengo.
“Nawaagiza Fuatilieni suala la kupokea Rushwa baina ya wafanyakazi wenu hasa pale wanapokwenda kufanya vipimo na kukadiria Majengo,”Ameeleza Balozi Amour
Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) Mbunifu Majengo Edwin John Nnunduma, amesema kuwa Bodi hiyo ina Watumishi wa kudumu 42 na Watumishi wa Mikataba 16 ambao wanafanya jumla ya Watumishi wa Bodi kuwa 58 na kwa mujibu wa Muundo mpya wa Bodi, IKAMA ya Bodi inatakiwa kuwa na Watumishi 114 hivyo kuna upungufu wa Watumishi 56.
“Kikao cha Faragha cha Bodi
Madhumuni ya Kikao cha Faragha ni kutekeleza maelekezo ya Mhe. Prof.Makame Mnyaa Mbarawa (Mb) Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi aliyoyatoa katika kikao cha faragha kati ya Menejimenti ya Wizara na Menejimenti ya
Taasisi zilizo chini yake kilichofanyika kuanzia tarehe 10 hadi 12 Juni, 2023 Beach Resort Hotel jijini Tanga. Kikao hiki kitaainisha hali na mazingira ya utendaji kazi wa Watumishi wa Bodi pamoja na kubainisha Watumishi ambao hawaleti tija katika utendaji kazi,”ameeleza Nnunduma
Nnunduma amebainisha matarajio ya Utendaji kazi Kwa watumishi wa Bodi hiyo baada ya Kikao kuwa ni kutoa majibu sahihi na kwa wakati,kuwa wawazi katika utendaji,kumjali na kumheshimu mteja,matumizi sahii ya taarifa za Bodi na Serikali,kuzingatia viwango, weledi na maadili ya taaluma,kuzingatia huduma inayotolewa inaendana na thamani ya fedha zinazotumika,kuwa tayari kujifunza na kubadilika, na Kutoa huduma kwa kutumia Teknolojia ya Kisasa.
Naye Kiongozi wa kanda kanfa ya Kati,Msanifu majengo kutoka (AQRB) Joseph Ringo amesema kazi kubwa inayofanywa na bodi hiyo ni kufanya ukaguzi kwenye miradi ya ujenzi hivyo ametoa wito kwa washitili kutumia wasanifu majengo waliosalijiliwa kwa leo na nia ya kuleta tija suala la ujenzi.
Sambamba na hayo kwa upande wake Mkaguzi wa Ndani wa AQRB Farha Hussein Baabde amesema suala la uadilifu, uchapakazi na uaminifu katika sehemu za kazi ni muhimu kwa watumishi kwani inaleta tija katika uchapakazi serikalini.
Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (Architects and Quantity Surveyors Registration Board) ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na.16 ya mwaka 1997 ambayo tarehe 01 Oktoba, 2010 ilifutwa na nafasi yake kuchukuliwa na Sheria Na. 4 ya mwaka 2010 ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi. Baada ya Bodi kuanzishwa, mwaka 1998 ilisajili Wataalam 188 na Kampuni 53. Hivi sasa Bodi ina Wataalam 1,340 na Kampuni 460.