CHAMA cha Waandishi wa Wahabari Wanawake Tanzania, Zanzibar, (TAMWA- ZNZ) kinawapongeza Mheshimiwa Jaji Aziza Iddi Suwedi na Bi Halima Mohamed Said kwa kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
Pongezi hizi zinakuja kufuatia uteuzi uliofanywa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi hivi karibuni baada ya kuteua wajumbe wapya wa Tume hiyo yenye jukumu la kusimamia Uchaguzi mkuu wa Zanzibar.
Tume ya uchaguzi hiyo imehusisha wajumbe saba, watano wakiwa ni wanaume akiwemo Mwenyekiti Jaji George Joseph Kazi, hivyo kuwa na wanawake wawili sawa na asilimia 28.6 na wanaume kuwa ni asilimia 71.4.
TAMWA-ZNZ inawatakia kila la kheri wajumbe hao wanawake na kuwaomba wasimamie maslahi ya wanawake katika uchaguzi ikiwemo kuweka mifumo ya kuripoti udhalilishaji/Ukatili wa Wanawake katika Siasa (VAWP), usalama wa wanawake katika uchaguzi na kupinga vita masuala ya rushwa na matumizi mabaya ya fedha katika uchaguzi.
TAMWA-ZNZ pia kwa kutambua maendeleo haya ya Tume kuwa na wanawake wawili kinyume na miaka ilivyopita kuwa na mwanamke mmoja ama hapana inampongeza Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi hizi.
Vile vile, TAMWA-ZNZ inapenda kukumbusha kuwa Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Tanzania imeridhia mikataba mingi ya kikanda na kidunia kuleta usawa wa kijinsia katika vyombo vya maamuzi.
Hivyo, ni muhimu sana kwa mamlaka za uteuzi kuhakikisha kuwa zinateua wanawake na wanaume kwa usawa wa 50/50 ili kuweza kufikia usawa wa kijinsia na hivyo kuwatia nguvu watoto wa kike kuwa wana nafasi sawa katika nchi yao na pia kwenda sambamba na idadi ya watu nchini ambapo kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 wanawake ni zaidi ya asilimia 50.
Hali kadhalika, azimio la 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililotolewa tarehe 31 Oktoba mwaka 2000 linasema. “Kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi kunakuza demokrasia ya nchi, uchumi, amani na utulivu kwa muda mrefu”.
Aidha, Mkataba wa kimataifa unaopinga aina zote za udhalilishaji dhidi ya wanawake, (CEDAW) wa mwaka 1979 katika kifungu cha 7 unasisitiza kuwa na haki sawa baina ya mwanamke na mwanamme katika uchaguzi na mchakato mzima wa upigaji kura na kuchaguliwa kushika madaraka.