Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi akiongoza Matembezi na mbio fupi za Uzazi Ni Maisha Wogging 2023 yalioanzia viwanja vya Butros Kiembe Samaki na Kumalizikia Viwanja vya Maisara Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amezipongeza jitihada zinazochukuliwa na wadau wa maendeleo, wahisani na mashirika kwa juhudi wanazozichukua katika kuiunga mkono serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana katika viwanja vya Maiasra vilivyopo Zanzibar alipokuwa akizungumza kwenye kampeni ya ‘ Uzazi ni Maisha Wogging Marathon (Walk-Jog-Run) kwa mwaka 2023 “ iliyoandaliwa kwa ushirikiano baina ya wizara ya Afya Zanzibar na Shirika la Kimataifa la Amref Health Africa Tanzania chini ya udhamini wa benki ya Absa.
Alisema wadau wa maendeleo na mashirika yana mchango mkubwa katika kusaidia maendeleo ya jamii na kulipongeza shirika la Amref Tanzania kwa kuanzisha kampeni ya ‘Uzazi ni Maisha Wogging yenye lengo la kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akilishukuru shirika la Amref Health Africa Tanzania pamoja na Mdhamini wa Matembezi na mbio fupi hizo benki ya Absa na wadau wake wote Mara baada ya kumaliza kampeni ya Uzazi ni Maisha wogging Zanzibar.
“Napenda niwashukuru Amref Health Africa kwa kutoa msaada wa gari maalum ambayo itasaidia kusafirisha wataalamu, kusafirisha sampuli, kutoa huduma za upimaji na ushauri nasaha kwa wananchi katika vituo vya afya hapa Zanzibar”, alisema.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Amref Health Africa, Githinji Gitahi (Wa pili kushoto) akikabidhi gari kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi
Dkt. Mwinyi alibainisha kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina mikakati ya kuzikabili changamoto zinazosababisha vifo vya mama wajawazito na watoto, hivyo kampeni hiyo ya AMREF itasaidia na kufanikisha kwa malengo.
Alibainisha kuwa hivi sasa kiwango cha vifo vya mama wajawazito na watoto kipo juu hapa Zanzibar, hivyo kampeni ya ‘Uzazi ni Maisha’ ya Amref Tanzania itasaidia kuliondosha tatizo hilo.
Alisema takwimu za mwaka 2017, zinaonesha vifo vya kina mama 134 kati ya vizazi hai 100,000 kwa mwaka na vifo 28 vya watoto wachanga kati ya vizazi hai 1,000, ambapo husababishwa na changamoto za huduma duni za mama na mtoto katika hospitali na vituo vya afya zikiwemo uhaba wa wahudumu a tatizo la kukosekana kwa dawa.
Dkt. Mwinyi, alieleza matumaini yake kupitia kampeni hiyo, kwamba serikali itaongeza vifaa tiba kwa vituo vya afya 28, sawa na asilimia 40.5 ya vituo vote 69 vinavyotoa huduma za mama na mtoto Zanzibar.
Pia, alieleza jitihada za serikali kumarisha huduma za afya ya msingi kwa ajili ya uzazi salama, italeta mafanikio makubwa ya kulinda maisha ya mama na mtoto.
Akizungumza kwenye hafla hivo, Naibu Waziri wa Afya, Hassan Khamis Hafidh, alisema lengo la kuanzishwa kwa kampeni ya “Uzazi ni Maisha” ni kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto nchini.
Naibu Waziri wa Afya, Hassan Khamis Hafidh
Alisema, katika kulikabili tatizo hilo kivitendo, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mikakati ikiwemo kuwachukulia hatua kali za kisheria na nidhamu watumishi wote wa sekta ya afya wanaokiuka sheria na taratibu za utumishi kutokana na uzembe kazini.
Aidha alisema serikali haitovumilia kauli chafu kutoka kwa watendaji wa sekta ya afya, utovu wa nidhamu unaosababisha athari mbaya kwa mama na watoto hasa wakati wa kujifungua.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania, Zlatan Milisic alisema “Tunashukuru kwa kupata fursa ya kuwa sehemu ya hafla hii iliyoandaliwa na Amref na wizara ya afya Zanzibar, michango itokanayo na mpango huu wa Uzazi Ni Maisha Wogging wa kuchangisha fedha yatakwenda katika ununuzi wa vifaa tiba ili kuboresha huduma za afya na kuokoa maisha ya mama na mtoto Zanzibar.
Wakati maendeleo yamepatikana, bado kuna kazi kubwa ya kupunguza viwango vya vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga. Umoja wa Mataifa bado una nia ya dhati ya kusaidia Tanzania na Zanzibar katika jambo hili muhimu.Kwa pamoja tunaweza kuleta mabadiliko na kutoa huduma bora za afya na matunzo kwa akina mama na watoto wachanga.” alisema
Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania, Zlatan Milisic
Naye, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Amref Health Africa kwa upande wa Tanzania, Dkt. Florence Temu, alisema lengo la kuanzishwa kampeni hiyo ya “Uzazi ni maisha ni kukusanya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kununuliwa vifaa tiba vya hospitali na vituo vya afya 28 vinavyotoa huduma za mama na mtoto, Zanzibar.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Amref Health Africa Tanzania, Dkt. Florence Temu
Alisema, wakiwa kwenye mwaka wa pili wa kampeni yao, Shirika la Amref Health Africa tayari limefanikiwa kukusanya shilingi milioni 557 na wamepokea ahadi za shilingi milioni 883 ambayo itafikisha lengo la kampeni hiyo kufikia 2024.
Kampeni ya “Uzazi ni Maisha” ilianza mwaka jana na inatarajiwa kukamilika mwakani inatekelezwa kwa kaulimbiu isemayo” changia vifaa tiba kwa uzazi salama” ambayo imechangia kufikia malengo ya kuanzishwa kwake mwaka wa pili sasa wa utekelezaji wake.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa, Obedi S. Laiser alisema ushirika kati ya Amref na Absa ulikuwa na thamani kubwa na kiasi kilichochangwa na benki ni mwendelezo wa juhudi za benki hiyo katika kutimiza sera yake ya kurudisha kiasi cha faida Kwa jamii (CSR) kunakosukumwa na utayari wa kushirikiana na jamii ambako benki inatoa huduma ili kuimarisha sekta ya afya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa, Obedi S.Laiser
Matukio katika Picha
Mgeni Rasmi, RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiongoza na kuambatana na viongozi wengine wa serikali na taasisi mbalimbali katika matembezi na mbio fupi za Uzazi ni Maisha Wogging 2023 Zanzibar, 26/08/2023
Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania, Zlatan Milisic akipokea cheti cha shukrani kutoka kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi mara baada ya matembezi na mbio fupi za Uzazi Ni Maisha Wogging 2023 zilizofanyika Zanzibar mwishoni mwa wiki iliyopita kwa lengo la kuchangisha vifaatiba kwa uzazi salama.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa, Obedi S.Laiser (Wapili kulia)ambayo benki ya Absa ndio wadhamini wakuu wa Matembezi na mbio fupi za Uzazi ni Maisha Wogging 2023, akipokea cheti cha pongezi kutoka kwa Mgeni Rasmi, RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi
Afisa Mkuu Mtendaji wa Amref Health Africa, Githinji Gitahi (Wa pili kushoto) akikabidhi gari kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya Vifaa Tiba kutoka kwa wadau mbalimbali wakati akiongoza Matembezi na mbio fupi za Uzazi Ni Maisha Wogging 2023 yalioanzia viwanja vya Butros Kiembe Samaki na kumalizikia Viwanja vya Maisara
Wananchi mbalimbali wakati wa hitimisho za Matembezi na mbio fupi za Uzazi ni Maisha Wogging katika viwanja vya Maisara, Zanzibar. Matembezi hayo yenye Kauli mbiu “Changia Vifaa Tiba kwa Uzazi Salama.
Picha ya pamoja kati ya Mgeni Rasmi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi na wadau mbalimbali waliochangia vifaa Tiba kwa Uzazi Salama katika programu ya Uzazi ni Maisha Wogging 2023 ikiwemo ( Mdhamini Mkuu Benki ya Absa; M & D Chemical & Surgical Ltd, Tanzania Ports Authority, NMB Bank, ITV/ Radio One, Swahili Sweatshop, Dalberg Tanzania, Siemens Healthcare LLC, benki ya CRDB, Strategis Insurance, NBC na kila mmoja aliyewezesha Programu ya Uzazi ni Maisha Wogging Marathon (Walk-Jog-Run) kwa mwaka 2023 kufanikiwa.