Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Kawajika Mwinyipembe akimpima jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO) mkazi wa Arusha aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH) wakati wa kambi maalum ya upimaji na matibabu ya moyo iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa afya JKCI na wenzao wa MRRH na kumalizika leo Mkoani Kilimanjaro. Jumla ya watu 700 wamepatiwa matibabu katika kambi hiyo.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth Mmari akimpa maelekezo ya namna ya kutumia dawa mkazi wa Kilimanjaro aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH) wakati wa kambi maalum ya upimaji na matibabu ya moyo iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa afya JKCI na wenzao wa MRRH na kumalizika leo Mkoani Kilimanjaro. Jumla ya watu 700 wamepatiwa matibabu katika kambi hiyo.
Afisa Uuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH) Zaituni Mbowe akimpima urefu na uzito mkazi wa Kilimanjaro aliyefika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH) kwaajili ya kupima moyo wakati wa kambi maalum ya upimaji na matibabu ya moyo iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa MRRH na kumalizika leo Mkoani Kilimanjaro. Jumla ya watu 700 wamepatiwa matibabu katika kambi hiyo.
Afisa lishe wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH) Ester Wazoel na mwenzake kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Faraji wakitoa elimu ya lishe kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani waliofika katika Hospitali ya Mawenzi kwaajili ya kipima moyo wakati wa kambi maalum ya uchunguzi na matibabu ya moyo iliyomalizika leo mkoani Kilimanjaro.
Picha na: JKCI
Na: Mwandishi Maalum – Kilimanjaro
Watu 700 wafanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo katika kambi maalum ya siku tano iliyokuwa ikifanywa na madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hosptiali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi (MRRH).
Kambi hiyo iliyomalizika jana Mkoani Kilimanjaro imekuwa na mwitikio mkubwa kuliko ilivyotarajiwa ukilinganisha na uwezo wa mabingwa hao kutoa huduma kwa watu waliojitokeza.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kufunga kambi hiyo Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo alisema kupitia kambi hiyo wameona uhitaji wa huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani ni mkubwa hivyo kuiomba Serikali kuangalia namna ya kusambaza huduma hizi na kuzisogeza kwa wananchi.
Dkt. Pedro alisema asilimia 55 ya wagonjwa watu wazima waliowaona walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu, huku wengine wakiwa na magonjwa ya kuziba mishipa ya moyo, magonjwa ya valvu na magonjwa ya umeme wa moyo kutokufanya kazi vizuri hivyo kuwapa rufaa wagonjwa 70 kufika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwaajili ya matibabu zaidi.
“Tulichogundua hasa katika jamii ya watu wa Kilimanjaro ni pamoja na watu wengi kuwa na uzito mkubwa, kuwa na matumizi makubwa ya chumvi na mafuta mengi lakini pia sababu za kijenetiki za familia kuwa na historia ya kuwa na magonjwa ya sukari na shinikizo la damu hivyo baadhi ya watu katika familia kurithi magonjwa hayo”,
“Wito wetu kwa jamii ni kuwa na tabia ya kuchunguza afya zao pale wanapoona dalili na wale ambao tayari wana magonjwa yasiyoambukiza wafanye vipimo vya kuchunguza moyo kwani utakapogundua tatizo mapema matibabu huwa rahisi na matokeo ya matibabu huwa mazuri zaidi”, alisema Dkt. Pedro
Akizungumza kuhusu watoto waliotibiwa katika kambi hiyo Daktari bingwa wa watoto kutoka JKCI Parvina Kazahula alisema jumla ya watoto 42 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo ambapo watoto 16 waligundulika kuwa na matatizo ya moyo.
Dkt. Parvina alisema watoto 12 walikuwa na magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu kwenye moyo pamoja na mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye mapafu kuwa na hitilafu, huku watoto wengine wanne wakiwa na matatizo ya valvu zao za moyo matatizo ambayo wameyapata wakati wa ukuaji.
“Wanawake tunatakiwa kuhudhuria kliniki ili kuweza kufuatilia vitu muhimu wakati wa ujauzito kupunguza athari za kupata watoto wenye magonjwa ya moyo, pia watoto wanaozaliwa wakiwa na dalili za magonjwa ya moyo wafikishwe hospitali mapema ili kuweza kutatua matatizo kwa wakati”, alisema Dkt. Parvina
Dkt. Parvina alisema mtoto anayezaliwa na magonjwa ya moyo huwa na dalili za ukuaji hafifu, kutokuongezeka uzito, kushindwa kupumua vizuri, kuwa na rangi ya bluu sehemu za mdomo na vidoleni.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi Dkt. EdnaJoy Munisi aliwapongeza wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kwa kuwa na mwitikio mkubwa wa kuchunguza afya zao na kuwataka wananchi hao kuzingatia ushauri wa wataalamu walioupata katika kambi hiyo.
“Nawaomba wananchi wa Kilimanjaro kuendelea kuwa na tabia ya kupima afya zenu hata baada ya kambi hii kwani hapa Mawenzi tunayo kliniki ya matibabu ya magonjwa ya ndani ikiwemo magonjwa ya moyo hivyo msisite kufika kwa ajili ya kupatiwa matibabu”, alisema Dkt. EdnaJoy
Aidha Dkt. EdnaJoy amewataka wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kupunguza matumizi makubwa ya chumvi, pombe na nyama nyekundu bali wazingatie ulaji wa mlo sahihi kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.
Naye mwananchi aliyepatiwa matibabu katika kambi hiyo Theresia Sangawe ilishukuru kwa kupata nafasi ya kupima moyo wake katika kambi hiyo na kukutwa yuko salama.
“Leo nilikuja hapa Hospitali kwa ajili ya kliniki yangu ya shinikizo la damu lakini nikapata nafasi ya kupima sukari kwenye damu na kupima moyo, nashukuru moyo wangu umekutwa uko vizuri, kuta za moyo ziko vizuri, na mishipa ya damu pia iko vizuri”, alisema Theresia
Theresia alisema kambi za matibabu ya kibingwa zikisogezwa kwa wananchi kama ilivyokuwa ya magonjwa ya moyo kutatoa motisha kwa jamii kuwa na shauku ya kupima afya zao.