Na Mwandishi wetu, Ruangwa
WACHIMBAJI wa Madini Mkoani Lindi wameiomba Serikali kuongeza nguvu ya umeme hasa katika maeneo ya migodi Ili kuongeza kasi ya utendaji kazi katika uzalishaji wa madini mkoani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari mojawapo ya Kampuni ya wachimbaji wa madini mkoani humo amesema licha ya changamoto hiyo pia kuna changamoto ya barabara kuelekea katika migodini.
Meneja wa Kampuni ya uchimbaji Madini ya Elianje iliyopo katika Kijiji cha Chingungwe wilaya ya Ruangwa Philbert Massawe amesema changamoto hizo ni miongoni mwa mambo yanayodhoofisha shughuli za uchimbaji katika maeneo yao.
Kufuatia hali hiyo ameiomba Serikali kutatua changamoto hizo Ili kuongeza tija katika sekta ya madini mkoani Lindi na Taifa kwa ujumla.
“Changamoto tuliyonayo ni kwamba licha ya sekta ya uchimbaji Madini nguvu ya nishati ni muhimu sana, lakini nguvu ya umeme ni ndogo, barabara nazo ni changamoto,” amesema Massawe.
Kufuatia hali hiyo ameiomba Serikali kuhakikisha kunakuwa na umeme wa uhakika na wenye nguvu ya kutosha na kuhakikisha barabara zinapitika muda wote.
Vile vile ameiomba Serikali iendelee kuleta maonyesho katika mkoa huo ili kutangaza fursa zinazopatikana zikiwemo za ajira.
Amesema, kampuni hiyo inayojishughuli na uchimbaji wa madini ya dhahabu, vito graphite, copper, chuma na Nikel amesema sekta ya madini ni miongoni mwa sekta zinazochangia kutatua tatizo la ajira nchini na huku akiwasihi vijana na wananchi kwau jumla kujitokeza kuchangamkia fursa hizo hasa katika kampuni yao.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa kuleta maonesho haya mkoani Lindi hatua hii itapelekea wadau na madini yanayozalishwa mkoani humo kujulikana maeneo yote, lakini pia yanachangia kutangaza fursa mbalimbali zikiwemp za ajira,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine amesema makampuni ya madini yanachangia mambo mbalimbali ya kijamii hasa katika sekta za Elimu, Afya na Maji huku akisema Kampuni ya Elianje imeweza kunufaisha jamii kwa maana ya kutengeneza ajira kwa sababu kuna vijana wengi ambao familia zao mpaka sasa zinanufaika kutokana na ajira ambazo wamezipata kutoka kampuni yao.
“Pia tumeshiriki katika sekta ya Elimu kwa kujenga madarasa katika Kijiji cha Chingungwe lakini pia tumefanya ukarabati wa madarasa yaliyokuwa yameharibika lakini pia katika suala zima la ulipaji kodi wanashirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambao ni wasimamizi wa mali zinazopatikana pamoja na kipato kwa maana ya kuhakikisha kile kinachostahili kulipwa katika maeneo ya kodi vyote vinasimamiwa katika utaratibu sahihi.