Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dkt Suleiman Serera na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Gracian Max Makota wamekutana na wadau wa madini ya Tanzanite kujadili mikakati ya kusaidia jamii inayowazunguka (CSR).
Kutokana na hali hiyo viongozi na wamiliki wa migodi wameanza mikakati ya kumaliza malalamiko ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani kukabiliana na umasikini na ukosefu wa miundombinu ya elimu, afya na maji.
Licha ya uwepo wa machimbo ya madini ya Tanzanite kwenye eneo hilo, ambayo hayapatikani sehemu nyingine duniani lakini bado miundombinu mingi ni ya hali ya chini.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dkt Suleiman Hassan Serera amesema japokuwa baadhi ya wamiliki wamechangia maendeleo ya maeneo wanayoyazunguka inabidi wengine nao watimize hilo.
“Kuchangia maendeleo kwenye maeneo yanayowazunguka ni takwa la kisheria inawabidi wengine ambao hawajatimiza takwa hilo wafanye hivyo,” amesema Dkt Serera.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Max Makota amesema wadau wa madini wanaotaka kusaidia jamii inayowazunguka wanapaswa kuonana na ofisi yake ili wapange maeneo ya kusaidia.
“Tupeane ushirikiano kwani ofisi yetu ipo wazi muda wote tushirikiane kufanya kazi kwa lengo la kusaidia jamii inayozunguka kwenye maeneo yetu ya machimbo,” amesema Makota.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (Marema) Justin Nyari amesema wachimbaji wamekuwa wakisaidia jamii inayozunguka katika sekta mbalimbali.
“Tumekuwa tukichangia maendeleo mbalimbali kwa jamii inayotuzunguka na kuwekeza sehemu tofauti ikiwemo ujenzi wa shule,” amesema Nyari.
Mchimbaji mwingine Wariamangi Sumari Mezea amesema wachimbaji madini wengi wamechangia mno maendeleo ila hawajangazi ndiyo sababu hawatambuliki.
Mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite, Bilionea Saniniu Laizer ameshajenga shule na kuikabidhi serikali na mmiliki wa kitalu C kampuni ya Franone Mining LTD imetoa Sh47 milioni za kujenga korido ya chumba cha kuhifadhi maiti kituo cha afya Mirerani na Sh171 milioni za kujenga barabara ya kuelekea mgodini.