Afisa Utalii Mamlaka ya Usimamizi wa wamyama pori Tanzania TAWA Lusajo Nsweve Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati akihamasisha utalii wa wamyama pori hai huko viwanja vya Kashangae Paje Mkoa wa Kusini Unguja katika Tamasha la Kizimkazi linalotarajiwa kuzinduliwa Agosti 26 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi.
Na Rahima Mohamed, Asya Khamis Maelezo
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania (TAWA) imewataka wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi katika ufunguzi wa Tamasha la Kizimkazi ili kujionea wanyama pori mbalimbali kutoka Tanzania Bara.
Hayo yamesemwa na Afisa Utalii kutoka Mamlaka ya usimamizi wa wanyama Pori Tanzania (TAWA) Lusanjo Nsweve wakati akizungumza na Waandishi wa habari huko Paje Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema wanyama hao watakuepo kuanzia leo hadi tarehe 31 na wananchi watajionea wanyama hao mubashara ikiwemo nungunungu, simba, chui, fisi, pundamilia, ndege mbalimbali na kupata elimu pamoja na kujua tabia za wanyama hao.
Afisa Lusanjo amesema Wananchi wanaweza kupata elimu ya ufugaji wanyama pori kwa kutumia Mbuga au mashamba Ili kuongeza pato la taifa Nchini.
Aidha amesema sekta ya utalii ni muhimu sana katika nchi yetu hivyo kuwepo kwa wanyama hao Zanzibar kutasaidia kuvitangaza vivutio mbalimbali nchini ili wanachi na wageni wajionee kwa macho yao na kutembelea vivutio hivyo.
Vilevile afisa huyo amesema kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia Tamasha hilo kutasaidia kuhamasisha wenyeji na wageni kujionea vivutio hivyo kwa ajili ya kuutangaza utalii na kuongeza wageni.
Hivyo amewasisitiza na kuwatoa wasiwasi wananchi watakaotembelea maonesho hayo kwani wanyama hao wapo katika hali nzuri na wametunzwa kitaalamu na kuekwa kwenye vizimba ambavyo viko imara kabisa.
Nao wakaazi wa Paje wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea fursa za maonesho mbalimbali ikiwemo wanyama pori ikiwa ni kivutio cha utalii.