Umati wa watu waliofika kwa mganga wa Tiba asili na tiba mbadala anayefahamika kwa jina la Bi Naweza mkazi wa kijiji cha Semeni wilayani Tunduru ambaye anatibu magonjwa mbalimbali ikiwemo tezi dume na mabusha bila kufanya upasuaji.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Semeni ambaye hakufahamika jina lake akizungumza na umati wa wananchi waliofika kwa mganga wa tiba asili na tiba mbadala Bi Naweza kwa ajili ya kupata matibabu ya maradhi yanayowasumbua.
Mratibu wa tiba asili na tiba mbadala ambaye pia ni mratibu wa ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole,akizungumza na mamia ya wananchi waliofurika kwa mganga wa tiba asili na tiba mbadala Bi Naweza anayefanya shughuli za kutoa tiba kwa kutumia tiba asili katika kijiji cha Semeni wilayani humo.
Msaidizi wa mganga wa tiba asili na tiba mbadala Bi Naweza,Salum Mtingala akionyesha vikombe vya maji vinavyotumika wakati wa kutoa huduma ya tiba kwa wananchi wanaofika kupata huduma za matibabu kwa Bi Naweza.
Baadhi ya wananchi waliofika kwa mganga wa tiba asili na tiba mbadala katika kijiji cha Semeni Bi Naweza wakiwa katika foleni kwa ajili ya uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu wakati wa kampeni iliyofanywa na wataalam kutoka Hospitali ya wilaya Tunduru kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma.
Na Muhidin Amri,Tunduru
HOSPITALI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma,imezindua kampeni mpya ya kutokomeza ugonjwa huo kwa kutembelea kwenye vilinge(makambi) ya waganga wa tiba asili na tiba mbadala ijulikanayo kwa jina la Kilinge kwa Kilinge.
Kampeni hiyo,inakusudia kuwapata watu wote waliokatisha matibabu ya Hospitali na kuacha kumeza dawa ambao wamekimbilia kwa waganga wa tiba asili na kuwaibua wagonjwa wapya walioambukizwa ugonjwa huo ili waweze kuanzishiwa matibabu.
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya hiyo Dkt Mkasange Kihongole amesema hayo jana, kabla ya kuanza zoezi la uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu kwa wananchi waliokutwa wakipata matibabu kwa Mganga maarufu wa tiba asili na tiba mbadala Bi Naweza mkazi wa kijiji cha Semeni wilayani humo.
Alisema,kitengo cha kifua kikuu na ukoma imeamua kuzindua kampeni hiyo kwa kufika kwenye vilinge vya waganga hao kutokana na uwepo wa idadi kubwa wa watu kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini wanaofika ili kupata matibabu.
Mkasange alisema,kwenye vilinge vya waganga wa tiba asili ni miongoni mwa maeneo hatarishi ambayo watu wanaweza kuambukizwa ugonjwa huo kwa urahisi kwa sababu ni maeneo yanayopokea watu wenye magonjwa tofauti ikiwemo ugonjwa wa hatari wa TB.
Alieleza kuwa,kwa kawaida ugonjwa wa kifua kikuu unaambukizwa kwa njia ya hewa hivyo,mtu mwenye ugonjwa huo ambaye hajaanzishiwa matibabu ni rahisi kuambukiza wengine pale anapopiga chafya na kukohoa kama hakutakuwa na tahadhari yoyote.
Alisema kutokana na hali hiyo,Hospitali ya wilaya ya Tunduru kitengo cha kifua kikuu na ukoma imeanza kampeni hiyo ya kutoa elimu kwa waganga wenyewe,wasaidizi wao na wananchi wote wanaokwenda kwenye vilinge kwa ajili ya kupata matibabu.
Dkt Mkasange alisema,kampeni ya uchunguzi kwenye vilinge vya waganga wa tiba asili sambamba na zoezi la kutoa elimu ya ugonjwa huo ni endelevu ili kuwaepusha watu na waganga wenyewe kuambukizwa ugonjwa huo.
Msaidizi wa mganga wa Tiba asili na tiba mbadala Bi Naweza Salum Mtingala alisema,kwa siku wanapokea zaidi ya watu 2,000 kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini wanaofika kwa ajili ya kupata matibabu.
Alitaja huduma zinazotolewa na Bi Naweza ni upasuaji wa mabusha,tezi dume bila kutoka damu na magonjwa mengine kwa kutumia dawa za asili ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa watu wanaofika kwa mganga huyo.
Aidha Mtingala,ameipongeza Hospitali ya wilaya Tunduru kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma kupeleka elimu ya kifua kikuu na uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa huo kwani imesaidia wananchi wengi kufahamu na kuchukua tahadhari ili kuepuka kuambukizwa.
Ameiomba serikali kuwaunga mkono katika shughuli zao,kwa kuboresha miundombinu ikiwemo barabara na kupeleka huduma ya maji ili kuwawezesha wananchi kufika kwa urahisi katika eneo hilo lenye mkusanyiko mkubwa wa watu.
Juma Makumbusya,ameishukuru serikali kupitia wizara ya afya kupeleka elimu ya kifua kikuu kwa waganga wa tiba asili kwa kuwa itasaidia kuokoa maisha ya watu wengi ambao kwa muda mrefu wanaangaika kutafuta majawabu ya shida zao.
Hata hivyo,ameshauri serikali kuendelea kushirikiana na waganga wa tiba asili ambao jamii inawaamini na wamekuwa kimbilio kubwa kwa baadhi ya watu wanaosumbua na magonjwa mbalimbali.