Wananchi wa Mkoa wa Lindi wameishukuru Serikali baada ya kutangaza rasmi kuanza kwa ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mapema mwezi Desemba mwaka huu katika eneo la Gongo kata ya Jamhuri mkoani humo.
Wananchi hao wasema hayo Agosti 22,2023 walipokutana na kuzungumza na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia juu ya utekelezaji wa mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaofadhili ujenzi wa Kampasi hiyo.
Pia wameiomba Serikali kuhakikisha wakandarasi watakaotumika kujenga chuo hicho kuhakikisha wanatekeleza kazi hiyo kwa Weledi na kukamilisha kwa wakati ili Chuo kiweze kuanza kama ilivyopangwa huku wakishukuru kushirikishwa toka hatua za awali za mradi.
Akitangaza kuanza kwa ujenzi huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kujengwa kwa kampasi hiyo ni maelekezo ya Mhe. Rais kuhakikisha mikoa yote ambayo haina vyuo vikuu inajengewa kampasi za vyuo vikuu.
“Leo nimekuja kutangaza rasmi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimekamilisha taratibu za kikanuni na kisheria za kuanzisha kampasi, kutakuwa na kampasi ya chuo hicho hapa Lindi na kitaanza na wanafunzi 360 ,”amesema Prof. Mkenda
Ametaja mikoa mingine itakayojengewa kamapsi za Vyuo Vikuu kuwa ni Kagera, Mwanza, Shinyanga, Singida, Manyara, Tanga, Simiyu, Kigoma, Ruvuma, Rukwa Katavi, na Zanzibar (Institute of Marine Scince) na kwamba kampasi hizo zinajengwa na Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).
Waziri Mkenda amevitaka Vyuo vikuu vitakavyojenga kampasi hizo kuzielekeza kwenye kutoa mafunzo ya amali lakini pia kufanya tafiti. Aidha amekipongeza Chuo Kikuu kwa kukamilisha taratibu hizo lakini pia Mkoa wa Lindi kwa kutoa ushirikiano wa kuhakikisha ujenzi wa chuo hicho unaanza.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mkuu wa wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga ameishukuru Serikali kwa kuupatia Mkoa wa Lindi Kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwani ni jambo ambalo lilikuwa likisubiriwa kwa muda mrefu. Ameeleza kuwa tayari Mkoa umewezesha upatikanaji wa eneo zaidi ya ekari 492 na ameahidi kwa niaba ya Mkoa kutoa ushirikiano kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Mipango, Fedha na Utawala) Prof. Bernadetha Killian amesema kupitia mradi wa HEET Chuo Kikuu kimepata Dola za kimarekani milioni 47.5 kwa ajili ya kutekeleza mradi kupitia shughuli mbalimbali ikiwemo ujenzi wa kampasi mpya, kuandaa na kuboresha mitaala , kusomesha wahadhiri kwa kipindi cha miaka mitano ambapo amesema Kampasi ya Lindi itajikita zaidi katika masuala ya kilimo na ufugaji wa Nyuki na kuwa itakuwa na kituo Wilayani Ruangwa kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo na tafiti.
Prof. Killian ameishukuru Wizara kwa kukiamini Chuo hicho kutekeleza miradi huo ikiwa ni pamoja na Serikali ya Mkoa wa Lindi kwa ushirikiano katika kuanzisha kampasi hiyo.