Makamu Mkuu wa Chuo Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Professa Maulilio Kipanyula (Katikati), akiongea na menejimenti ya Taasisi ikiwa ndiyo kikao chake cha kwanza katika utekelezaji wa majukumu yake tangu kuteuliwa na Mkuu wa Chuo Bw. Omari Issa Agosti 14, 2023.
Makamu Mkuu wa Chuo Professa Maulilio Kipanyula ( kushoto) akifafanua jambo wakati wa kikao na Menejimenti ya Taasisi , kulia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango,Fedha na Utawala Professa Suzana Augustino.
Makamu Mkuu wa Chuo Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Professa Maulilio Kipanyula amekutana na Menejimenti ya Taasisi kwa lengo la kufahamiana pamoja na kutoa mrejesho wa kikao kazi cha watendaji wakuu wa Taasisi za umma ambacho Mgeni Rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kilichofanyika Agosti 19, 2023 jijini Arusha.
Akizungumza katika kikao hicho leo Agosti 22, 2023 Professa Kipanyula amesema kuwa mojawapo ya maazimio ya kikao hicho ni kuwa taasisi za umma kujitambua na kutekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za kuanzishwa kwake na kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipavyo ili kujenga Tanzania bora zaidi.
“Ili kuhudumia umma ni lazima kujua malengo ya uanzishwaji wa taasisi na manufaa kwa umma na kuhakikisha wananchi wanahudumiwa kwa haraka na wakati “ amesema Professa Kipanyula
Professa Kipanyula amewataka watendaji hao kuhakikisha kila mmoja anawajibika katika eneo lake la kazi na kuhakikisha utekezaji unafanyika kwa wakati ili kuleta matokeo chanya katika utendaji utakaongeza uzalishaji na kuinua uchumi wa nchi.
“Ni lazima tufanye kazi kimkakati kwa kusimamia lengo la kuanzishwa kwa taasii hii ili kutoa wanafunzi wenye ujuzi na tafiti nyingi zitakazo tatua changamoto zinazoikabili jamii” amesema Professa Kipanyula
Aidha, Professa Kipanyula ameongeza kuwa ni muhimu kuongeza ufanisi zaidi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuanzisha miradi mbalimbali pamoja na kupanua wigo wa ushirikiano na wadau kutoka nje ya nchi ili kuongeza udahili wa wanafunzi wa nje.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ubunifu Professa Anthony Mshandete alimshukuru Makamu Mkuu wa Chuo Professa Kipanyula kwa kukutana na Menejimenti na kuwataka watendaji hao kusimamia mawasiliano baina yao na wale wanawaongoza ili kuleta tija katika utendaji.
Kwa Upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Professa Suzana Augustino amemshukuru Makamu Mkuu wa Chuo Prof. kipanyula kwa mrejesho wa kikao kazi na kuitaka menejimenti kuongeza nguvu katika utendaji wao pamoja na kusimamia vyema eneo la huduma kwa wateja ili kutoa huduma iliyobora .