Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imefurahishwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kujenga hoteli kwa ajili ya kuongeza mapato na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, Stanslaus Mabula alipoongoza kamati hiyo kukagua miradi ya katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mabula ambae ni Mbunge wa Jimbo la Nyamagana alisema “kwanza niwapongeze sana Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kufikiria kuwa na vitega uchumi ambavyo kiukweli vitaipaisha halmashauri hii. Kamati tumefurahishwa kuona kwanza ile hoteli ya Jiji la Dodoma ambayo tayari imepata mwendeshaji sababu tunaamini halmashauri haiwezi kufanya kazi ya kuendesha hoteli vingenevyo itakuwa changamoto. Hiyo peke yake inawapa uhakika kwamba mradi mlionao tayari unawaingizia kipato. Sisi kama kamati tumekuwa na msisitizo kila wakati, kwanza kuhakikisha halmashauri zinaongeza mapato kwa kubuni vyanzo vingi zaidi ili ziweze kuongeza mapato mengi zaidi”.
Alisema kuwa imani ya kamati yake lengo kubwa la miradi ya uwekezaji wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni kulifanya jiji hilo liweze kujitegemea. ”Na majiji mengi bado hayana miradi ya namna hii. Dodoma ni Jiji changa lakini limekuja kwa kasi ya hali ya juu kwa hiyo tunawapongeza sana” alisema Mabula.
Akisoma taarifa ya mradi wa Hoteli ya Jiji la Dodoma (Best Western Dodoma City Hotel) Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo alisema kuwa hoteli hiyo ilijengwa kwa gharama ya shilingi 9,995,881,126.75. “Mradi huu umejumuisha miundombinu mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha utoaji wa huduma nzuri na za kisasa kwa wateja hali iliyofikia kuwa na hadhi ya nyota nne. Hoteli ina ghorofa 11, vyumba vya kulala 95 kati ya hivyo 63 ni vyumba vya kawaida ambavyo vinatumika. Vyumba vitatu ni ‘presidential suite’, kumbi tatu za mikutano migahawa mitatu, bwalo la kuogelea moja, chumba cha mazoezi, lifti tatu na eneo la maegesho ya magari” alisema Kayombo.
Akiongelea mafanikio ya mradi alisema kuwa ni kuongeza mapato kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Faida nyingine ni kutoa huduma za kijamii kwa wananchi wa ndani na nje ya Jiji la Dodoma. Mradi umetoa fursa za ajira kwa wananchi ambapo hadi sasa jumla ya wananchi 80 wameajiriwa” aliongeza Kayombo.
Ikumbukwe kuwa mradi wa hoteli ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ulianza kujengwa Mwezi Agosti, 2019 na kukamilika Aprili, 2023.