Timu ya kata ya Pasiansi imefanikiwa kupata sare dhidi ya Timu ya kata ya Nyamanoro kwa kufungana goli moja kwa moja mchezo uliochezwa katika uwanja wa Baptist Kona ya Bwiru wilayani Ilemela
Akizungumza kabla ya kuanza Kwa mchezo huo, Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Mwanza Ndugu Caroline Masanja amesema kuwa lengo la mashindano ya The Angeline Jimbo Cup 2023 ni kuibua vipaji na kufanya sekta ya michezo kama sehemu ya ajira kwa vijana hivyo kuwaasa kucheza mchezo wa amani na upendo
‘.. Tunaamini michezo ni furaha, michezo ni ajira lakini pia michezo hujenga urafiki, Niwaombe tucheze mchezo wa upendo ..’ Alisema
Aidha Ndugu Masanja amewataka wachezaji hao kufuata Sheria na taratibu za mpira wa miguu wakati wote wa mashindano ili kuepuka adhabu zisizo za msingi kwa timu zao
Kwa upande wake nahodha wa timu ya kata ya Pasiansi Abdallah Riziki amesema kuwa timu yake imepata nafasi nyingi za ushindi lakini wameshindwa kuzitumia vizuri kitendo ambacho kimewagharimu kushindwa kutoka na ushindi katika mchezo huo hivyo kuwaahidi mashabiki kufanya vizuri katika mchezo utakaofuata
Nae msemaji wa timu ya kata ya Nyamanoro ambae pia ni katibu wa siasa, itikadi na uenezi wa CCM wa kata hiyo Ndugu Shomari Kaswaka amesema kuwa mchezo wao wa leo ulikuwa na ushindani mkubwa huku akijisifu kwa kutekeleza ahadi aliyoitoa katika mchezo wake wa kwanza baada ya kufungwa magoli matatu kwa moja dhidi ya Kitangiri ya kuhakikisha anabadilisha benchi lote la ufundi na baadhi ya wachezaji ili timu yake iweze kupata matokeo mazuri katika michezo inayofuata
Kabla ya tamati ya mchezo wa Leo timu ya Nyamanoro ndio iliyokuwa ya kwanza kuzichungulia nyavu za timu ya kata ya Pasiansi na baadae timu ya kata ya Pasiansi kufanikiwa kusawazisha kwa mkwaju wa penati baada ya mchezaji wa timu ya kata ya Nyamanoro kufanya makosa