Na Mwandishi wetu, Ruangwa
NAIBU Waziri wa Madini Dk Stephen Kiruswa amezindua maonyesho ya madini na fursa za uwekezaji Mjini Ruangwa Mkoani Lindi, kwa kuelezea kuwa wamejipanga kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha madini kwa kusafirisha bidhaa na siyo malighafi.
Dk Kiruswa ameyasema hayo mjini Ruangwa mkoani wakati akiwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa maonyesho ya madini na fursa za uwekezaji.
Hata hivyo, amewataka wawekezaji wakubwa kujenga mitambo ya kuchakata madini kwani yataongezeka thamani pindi yakisafirishwa nje ya nchi yakiwa bidhaa na siyo malighafi.
“Kwenye madini hatutaki kuona kuwa tunazalisha malighafi, tunapaswa kuwa na bidhaa ambayo itakuwa inaongeza thamani ya madini kuliko inavyofanyika hivi sasa,” amesema Dk Kiruswa.
Pia, amewataka wawekezaji wasijifiche kwenye vivuli vya utafiti kwani wanapaswa kuanza kazi pindi wakifanya utafiti kuliko kutumia muda mrefu.
“Mnapomaliza utafiti fanyeni kazi kwani utafiti wa madini ya kinywe unapopewa miaka tisa ya utafiti isige kigezo cha ucheleweshwaji fanyeni kazi mara baada ya kuchukua vibali,” amesema Dk Kiruswa.
Mkuu wa mkoa wa Lindi, Zainab Tellak amesema maonyesho ya madini na fursa za uwekezaji zitafanyika kwa muda wa siku sita kuanzia Agosti 21 hadi Agosti 26.
“Kauli mbiu ya maonyesho haya ni wekeza Lindi kwa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii,” amesema Tellak.
Mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma amesema wawekezaji wazalendo wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi tofauti na wawekezaji wa nje kwani
“Mnapopewa vibali vya utafiti ninyi mnaojiita wawekezaji wakubwa wa nje mnatumia muda mrefu tofauti na wawekezaji wazalendo, chimbeni madini mtajirike na serikali ipate kodi,” amesema Ngoma.
Meneja uwezeshaji wachimbaji wadogo wa shirika la madini la Taifa (Stamico) Tuna Bandoma, amesema serikali imejipanga kuboresha uchimbaji wa madini ya chumvi.
Mbunge wa kuteuliwa na Rais, Riziki Said Lulida amesema wachimbaji wadogo wanapaswa kupewa kipaumbele na siyo kunyang’anywa maeneo yao na kufukuzwa pindi wakiyagundua.
“Wachimbaji wadogo kwa asilmia kubwa ndiyo wavumbuzi wa madini maeneo mbalimbali nchini hivyo wapewe kipaumbele na siyo kufukuzwa au kunyang’anywa maeneo yao,” amesema Lulida.