ZAO la korosho ni miongoni mwa mazao ya kimkakati la biashara yanayotegemewa katika kukuza uchumi wa Taifa kutokana na kuliingizia Serikali fedha za kigeni.
Mbali na kutegemewa na Taifa pia ni zao kuu la biashara kwa wananchi wa mikoa ya kusini pamoja na mikoa mingine ambayo kwa sasa imeanza kulima zao hilo.
Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikiuza korosho ghafi na hivyo kulikosesha Taifa baadhi ya mapato pamoja na ajira ikilinganishwa na kuuza korosho iliyobanguliwa.
Hivi karibu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alifanya ziara mkoani Mtwara pamoja na mambo mengine aliwasisitiza wakulima wajipange kuuza korosho iliyobanguliwa ili kuongeza tija.
Mheshimiwa Majaliwa alisema kuwa Serikali imedhamiria kufufua viwanda vya kubangua korosho lengo likiwa ni kuliongezea thamani zao kwa mkulima na Taifa kwa ujumla.
Alisema kitendo cha kuuza korosho ghafi kinalikosesha Taifa na wakulima mapato, hivyo inataka manufaa yote yatokanayo na zao la korosho yabaki nchini.
“Wakati wa kubadilika umefika, tutumie fursa hii kujenga viwanda vya kubangulia korosho na kuwawezesha wakulima kubangua na kuuza katika masoko ya nje na ndani.”
Waziri Mkuu alisema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anahitaji kuona Tanzania inauza korosho zilizobanguliwa nchini badala ya kuuza korosho ghafi.
“Hivyo, wakulima wa zao la korosho fanyeni kilimo cha kibiashara kwa kuacha kuuza korosho ghafi na badala yake muuze korosho zilizobanguliwa ambazo zimeongezwa thamani.“
Alisema kilo moja ya korosho iliyobanguliwa ni takribani shilingi 13,000 na ghafi ni shilingi 2,000, ukibangua kilo nne za korosho ghafi unapata kilo moja ya ya korosho iliyobanguliwa.
Alisema kitendo cha kusafirisha korosho ghafi nje ya nchi kinawakosesha baadhi ya mapato yakiwemo yatokanayo na maganda ya korosho ambayo yanatumika kutengenezea mafuta.
Aidha, Waziri Mkuu alitoa wito kwa wamiliki wa viwanda vya kubangua korosho watoe nafasi kwa wakulima kwenda kubangua korosho zao na kuwatoza gharama za ubanguaji.
“Wenye viwanda igeni mfano wa kiwanda cha kubangua korosho cha Organic Growth Limited (OGL) kilichopo Tandahimba ambacho kinaruhusu wakulima kwenda kubangua.”
Aidha, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaagiza watendaji wanaosimamia zao hilo wahakikishe wakulima wanapata pembejeo kulingana na mahitaji yao na kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda cha OGL Aldina Fakiri alisema wamejipanga ipasavyo kuhakikisha asilimia kubwa ya korosho inauzwa ikiwa imebanguliwa.
Alisema mapato mengi yanapotea kwa kuuza korosho ghafi, ambapo alitoa mfano wa maganda ya korosho ambayo yanatumika kuzalisha mafuta kwani ukiuza ghafi huyapati.
Aldina Fakiri alisema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kubangua tani 3,000 za korosho ikiwa ni sawa tani 720 za korosho zilizobanguliwa kwa mwaka.
Alisema kiwanda chao kitatoa fursa kwa wakulima kwenda kubangua korosho zao na kuwatoza gharama za ubanguaji. “Pia tutashirikiana nao katika kuwatafutia masoko.“
Alisema kiwanda ambacho kipo katika hatua za majaribio ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 3.5 kinatarajiwa kutoa ajira 200 kati yake 50 ni za kudumu na 150 zitakuwa za muda.
Kwa upande wao, wakulima wa zao la korosho waliishukuru Serikali kwa uamuzi wake huo wa kuendelea kuchochea ujenzi wa viwanda vya kubangulia korosho nchini.
Wakulima hao walisema uwepo wa viwanda utawawezesha kubangua korosho na kuziuza zikiwa zimeongezewa thamani badala ya kuuza korosho ghafi kama ilivyo sasa.
Alife Kajonje mmoja wa wakulima hao alisema ujio wa viwanda vya kubangulia korosho ni mkombozi kwa mkulima wa korosho na Taifa kwa ujumla kwani vinakwenda kuongeza thamani ya zao hilo, pia kupunguza tatizo la ajira.