Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeridhishwa na ujenzi wa Jengo la Kitega Uchumi Mtumba kwa shilingi bilioni 18 lililojengwa kwa lengo la kuongeza mapato ya ndani ya Halmshauri ya Jiji la Dodoma.
Kauli hiyo ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Stanslaus Mabula baada ya kupokea taarifa ya Jengo la Kitega Uchumi Mtumba la Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika ukumbi wa kisasa wa mikutano wa halmashauri hiyop.
Mabula alisema “Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, tumesikiliza taarifa zote tatu. Kwanza niwapongeze sana Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kufikiria kuwa na vitega uchumi ambavyo kiukweli vitaipaisha halimashauri hii. Sisi kama Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, tumekuwa na msisitizo kila wakati kwanza kuhakikisha halmashauri nchini zinaongeza mapato yake. Pili, zibuni vyanzo vingi zaidi ili ziweze kuongeza mapato mengi zaidi na tatu ni namna ya utumiaji wa mapato yenyewe. Nne kuangalia namna miradi inayotekelezwa tija yake ya sasa na ya baadae. Kwa miradi hii iliyotajwa na kwa maelezo yake Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma unaona kabisa ni miradi ambayo ina makusudi mazuri na lengo kubwa ni kuendelea kuifanya Halmashauri ya Jiji la Dodoma iweze kujitegemea”.
Alisema kuwa halmashauri hiyo inakuwa kwa kasi ikilinganishwa na halmashauri nyingine zenye hadhi ya jiji. “Na majiji mengi nchini bado hayana miradi ya namna hii nadhani hata ukienda Jiji la Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na Tanga. Dodoma ni Jiji changa lakini limekuja kwa kasi ya hali ya juu, kwa hiyo tunawapongeza sana na tunamatumiaini kwamba mtafika vizuri” alisema Mabula.
Aidha, alishauri miradi inayojengwa na halmashauri baada ya kukamilika atafutwe mwekezaji mwendeshaji. “Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa mradi wa aina hii na mingine mingi inayojengwa katika halmshauri, kamati mara nyingi imekuwa ikishauri baada ya kuwekeza atafutwe muendeshaji na halmashauri ibaki kukusanya mapato. Kwa hiyo Mstahiki Meya ni lazima uhakikishe anapatikana wawekezaji muendeshaji na hilo ndilo pendekezo letu namba moja kama kamati. Hii itafanya jitihada nzuri hizi zisije zikafifishwa ili ziendelee kuzaa matunda tunayoyakusudia” alisema Mabula.
Akiongelea ukumbi mkuwa wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wenye uwezo wa kubeba watu zaidi ya 1,000 alisema kuwa ni ukumbi bora. Alisema kwa kuwa eneo la Mji wa Serikali Mtumba bado jipya, muwekezaji muendeshaji ukumbi atauendesha kibiashara.
“Muendeshaji ukumbi hata matangazo yake yatakuwa kibiashara hivyo, atautangaza vizuri zaidi ukumbi huu na kuunganisha na hii hoteli ya Jiji ya Mtumba. Usishangae watu wanatoka Arusha na maeneo mengine kuja kufanya mikutano hapa na wakapumzika katika hoteli hii. Dodoma ni mji mkubwa unahitaji watu wengi na una fursa nyingi. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma hatuna mengi tuseme tu tumefurahishwa sana” alisema Mabula.
Akisoma taarifa ya mradi wa Jengo la Kitega Uchumi Mtumba, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo alisema kuwa mradi huo ulijengwa katika Mji wa Serikali Mtumba kama kielelezo katika Mji wa Serikali. “Mradi mzima una thamani ya shilingi 59,313,970,776.35. Ujenzi umegawanyika katika awamu mbili za utekelezaji. Awamu ya kwanza ujenzi wenye thamani ya shilingi 18,875,665,009.83 fedha kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ukihusisha jengo la ‘Tower B’ lenye ghorofa sita na jengo la kumbi za mikutano. Jengo la ‘Tower B’ linajumuisha sakafu ya chini yenye maeneo kwa ajili ya kutolea huduma za kibenki, mgahawa na eneo la mapokezi. Sakafu ya kwanza ina maeneo kwa ajili ya ofisi mbalimbali. Sakafu ya pili mpaka tano inachukuliwa na eneo la hoteli yenye vyumba vya kulala 66 na eneo la mgahawa” alisema Kayombo.
Akiongelea jengo la kumbi alisema linajumuisha ukumbi mmoja mkubwa wenye uwezo wa kukeba watu 1,000. “Kumbi ndogo sita zenye uwezo wa kubeba watu 50-100 na eneo maalum la VIP kwa ajili ya wageni maalum kupumzika. Kumbi zimekamilika na zimeanza kutumika. Mheshimiwa Mwenyekiti gharama za kukodi ukumbi huu mkubwa kwa kikao kimoja unalipa shilingi 5,000,000 na kumbi ndogo shilingi 500,000 hadi sasa kumbi zinafanya vizuri na shilingi 111,586,000 zimelipwa upande wa kumbi za mikutano” alisema Kayombo.
Ikumbukwe kuwa eneo la ujenzi lina jumla ya mita za mraba 35,152.4 na halmashauri ipo katika hatua za manunuzi ya kumtafuta muendeshaji wa Jengo la Kitega Uchumi Mtumba na zaidi ya kuongeza mapato ya halmashauri mradi utatoa fursa za ajira kwa wananchi wa Dodoma.