Ofisa mfawidhi wa LATRA Joseph Michael akizungumza na waandishi wa habari juu ya kupiga marufuku vyombo vya usafiri maarufu Kama daladala na Bajaji ndani ya mji wa Arusha.
Julieth Laizer,Arusha.
Mamlaka ya usafiri Ardhini (Latra) imezipiga marufuku magari madogo ya abiria na bajaji kufika katikati ya mji kuanzia jumatatu agosti 21 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Ofisa Mfawidhi wa Latra mkoa wa Arusha, Joseph Michael amesema kuwa maagizo hayo ni utekelezaji wa mpango wa serikali kwenye majiji yote.
“Katika kutekeleza sera ya serikali, inasema magari yanayofaa kuingia mjini yanatakiwa kuwa na uwezo wa kubeba abiria kuanzia 25 na kuendelea yaani Costa au mabasi makubwa. “amesema .
Michael ameongeza kuwa ,Utekelezaji huo umeanza kwenye majiji mbali mbali ambapo Arusha utaanza jumatatu hivyo kuanzia sasa hatutaendeleza leseni yoyote ya daladala kwenye ruti zinazoingia mjini.
Hata hivyo utekelezaji wa Mpango huo unakuja kipindi ambacho kumekuwepo na mgogoro mkubwa kati ya vyombo hivyo vya usafiri hadi kupelekea mgomo wa daladala uliosababisha adha kubwa ya usafiri kwa wakazi wa Arusha.
Mwenyekiti wa umoja wa madereva Bajaji jiji la Arusha, Shafii Ndalo amesema kuwa bado wanachama wao hawajaridhia swala hilo hivyo bado wanahitaji mda wa kutafakari.
“Hili swala bado tunahitaji kutafakari hivyo kwa sababu vikao vyetu vinaendelea tunaomba mda wa kupata maazimio na baadae tutazungumza na vyombo vya habari msimo wetu maana tunaona bado hatujatendewa haki kwani hatujakataa kuondoka kwenye ruti bali tunaomba vituo vya mjini viwepo maana huko wanapotupeleka hakuna abiria na vijijini kabisa hivyo Tunaomba tufikiriwe”amesema Shafii.
Nao Baadhi ya madereva bajaji wamesema kuwa ,kitendo cha wao kupangiwa kwenye vituo ambavyo hawakuvitaka wao ambavyo vipo nje ya mji kitakuwa kigumu sana kwani huko walipopangiwa hakuna abiria kabisa badala yake wataishia kufanya kazi za hasara wakati wanadaiwa marejesho ,hivyo wameomba kufikiriwa upya na kupangiwa maeneo ya mjini ambayo kuna abiria ili waweze kutimiza malengo yao kwani nao wana majukumu kama wengine .
Hivyo waliomba uongozi wa mkoa kukaa chini na viongozi wao na kuwasikiliza mahitaji yao ili kwa pamoja waweze kuelewana vinginevyo itakuwa ni ngumu sana wao kukubaliana na hayo matokeo huku ikilinganishwa kuwa kitengo hicho kimeajiri idadi kubwa ya vijana ambao wangekuwa mtaani bila kazi yoyote.