MKURUGENZI Mkuu Wakala wa Nishati Vijijini (REA),akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 18,2023 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya wakala huo na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2023/24.
MKURUGENZI Mkuu Wakala wa Nishati Vijijini (REA),akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari leo Agosti 18,2023 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya wakala huo na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2023/24.
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIKA Mwaka wa fedha 2023/24,Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imepanga kugawa mitungi ya gesi ya kupikia (LPG) 2,700 kila mkoa ili kuongeza matumizi ya nishati safi ambayo yatasaidia kulinda na kuhifadhi mazingira ambapo hekta 400,000 za misitu zinaharibiwa kila mwaka kutokana na shughuli za kibinadamu.
Hayo yamesemwa leo Agosti 18,2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy,wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya wakala huo na mwelekeo wa mwaka wa fedha 2023/24.
Mhandisi Saidy amesema kuwa lengo la serikali ni kubadili mitizamo ya wananchi katika matumizi ya nishati chafu ili kujikita katika matumizi ya nishati safi ya gesi na umeme ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kutaka taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 300 kuacha matumizi ya kuni na mkuu.
“Wakala, umeanza kutekeleza Mradi wa kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia kwa utaratibu wa utoaji ruzuku kuwezesha usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia (LPG) 71,000 yenye thamani ya Sh. bilioni tatu pamoja na majiko banifu 200,000 katika maeneo ya vijijini.
“Kwa mwaka wa Fedha 2023/24 jumla ya fedha takribani Sh. bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha mradi huo”amesema Mhandisi Saidy
Amesema , mradi mwingine ni ule wa kusambaza gesi asilia ya kupikia katika Mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani pembezoni mwa Mkuza wa bomba kuu la kusafirisha gesi asilia.
Vile vile, amesema utekelezaji wa Mradi huo utahusisha REA na TPDC kwa mwaka wa fedha 2023/24 na jumla ya Sh. bilion 20 zinatarajiwa kutumika.
“Mradi huu utahusisha ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi asilia (CNG) lenye urefu wa km 44.4 (Mnazi Mmoja – Lindi (km 22.9) na Mkuranga – Pwani (km 21.5) ambapo jumla ya nyumba/wateja 980 kunufaisha (Mnazi Mmoja – Lindi, wateja 451 na Mkuranga-Pwani, wateja 529)”amesema
Hata hivyo, amesema Serikali kupitia REA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) imetenga Dola za Kimarekani milioni sita kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa majiko banifu ya kupikia 200,000 katika maeneo ya vijijini na vijiji miji Tanzania bara.
Aidha amesema kuwa REA ipo katika mchakato wa kuanzisha vituo maalum kwa ajili ya kupima gesi vijijini zinazotumika kupikia majumbani ili kuwezesha wananchi wengi kutumia nishati hiyo na kuondokana na matuzi ya kuni na mkaa yenye athari kubwa kiafya,kimazingira na kiuchumi.
Mhandisi Saidy amesema katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini REA, imepanga kuhakikisha kuwa gesi inapatika katika maeneo ya vijijini kwa gharama ambazo mwanachi wa kawaida anaweza kuzimudu.
“Katika kufanikisha hilo hivi sasa Wakala wa Nishati Vijijini tupo katika mazungumzo na Kampuni ya PUMA ili kujenga vituo vya kupima gesi katika maeneo mbalimbali ili kuwezesha wananchi kupata hudumu kulingana na kiasi cha fedha walizonazo.
“Vituo hivi vya kupima gesi vitawezesha wananchi kupata huduma kwa fedha waliyonayo utakuwepo utaratibu ambao utawezesha mtu kupima gesi kwa fedha aliyonayo akitaka kilo moja anapata siyo kama ilivyo sasa mtu analazimishwa kununua kulinga na ujazo uliopo”amesema
Ameeleza kuwa wanaendelea na jitihada na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi na kuachana na matumizi ya nishati chafu katika maeneo mbalimbali nchini.
“Wananchi wamekuwa na hofu kuhusu upatikanaji wa nishati safi lakini pia bei yake lakini niwahakikishie kuwa gharama za matumizi ya gesi ni ndogo ukilinganisha na matumizi ya kuni na mkaa ambayo yanaathari kubwa kiuchumi,kiafya na kimazingira”amesema