NA STEPHANO MANGO, SONGEA
AFISA Elimu wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Frank Sichalwe amewataka wazazi na walezi wa watoto wanaosoma shule za msingi na awali kuchangia chakula shuleni ili kuinua kiwango cha elimu na kuboresha afya za wanafunzi hao.
Sichalwe ameyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake kuhusu umuhimu wa wazazi kuchangia chakula hicho ili kuleta ustawi wa afya za wanafunzi na kukuza taaluma katika halmashauri hiyo
Alisema kuwa tathimini ya utoaji wa chakula mashuleni sio nzuri kwani wanafunzi wanaopata chakula shuleni ni wachace sana, jambo ambalo ni kiashiria hatarishi kwa afya za watoto na zaidi ni kinyume na haki za binadamu.
Amewaagiza Maafisa Watendaji wa kata na mitaa kwa kushirikiana na Wenyeviti wa Serikali za mitaa kusimamia shule zilizo kwenye maeneo yao na kuhakikisha kila mzazi anawajibika kwa mtoto wake ili apate chakula cha mchana awapo shuleni na kuwachukulia hatua za kisheria wazazi wanaokaidi.
“Tumieni sheria ndogo za vijiji, kuwabana wazazi hao, kwani sera ya Elimu bila malipo imebainisha wazi, moja ya jukumu la mzazi ni kumpatia mtoto mahitaji binafsi ikiwemo chakula, vijiji visivyo na shetia ndogo hakikisheni mnazo ili kuwabana wazazi hao na watoto kupata haki yao ya msingi”. Amesisitiza Afisa Elimu huyo
Alisema kuwa ili kutilia mkazo suala la lishe kwa watoto na wanafunzi Serikali imeunda kamati ya lishe katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambayo inaongozwa na Afisa Elimu Msingi lengo ni kuhakikisha watoto wanapata haki yao ya msingi ya kupata chakula
Naye Afisa Lishe Manispaa ya Songea Alberth Semkamba Ametoa rai kwa jamii kuzingatia umuhimu wa siku 1000 za mwanzo za mtoto kuanzia utungaji mimba hadi kuzaliwa kwa mtoto kwani katika kipindi hicho mtoto atatakiwa kunyonyeshwa maziwa ya Mama pekee hadi pale tu atakapofikisha umri wa miezi sita.
Semkamba alisema kuwa wazazi wanatakiwa kutambua umuhimu wa lishe bora kwa watoto, na kwamba wanapaswa kutimiza jukumu hilo, kwa kutambua kuwa lishe bora ina nafasi kubwa ya ufaulu wa mwanafunzi katika masomo yake