Na.Elimu ya Afya kwa Umma.
Imeelezwa kuwa mpango wa utengenezaji wa kadi(Score Card) ina mchango mkubwa katika matumizi ya takwimu kutokomeza Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele (NTD’s)katika jamii ikiwemo matende na mabusha pamoja na vikope.
Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Mkurugenzi Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe katika ufunguzi wa Kikao cha kuwajengea uwezo kuhusu Kadi ya Alama (Score Card) Waratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Tanzania bara (RNTDCo) ngazi ya mkoa ambayo yameratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya ALMA.
Dkt. Kapologwe amesema amesema Kadi ya alama (Score Card) itakuwa shirikishi katika kuendelea kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele huku akitoa rai kwa watumishi kutoka Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuweka mkazo katika matumizi ya takwimu katika kuandaa mipango inayoakisi uhalisia katika mapambano ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.
“Hii itarahisisha sana uandaaji wa takwimu katika mapambano ya magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele lakini serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele katika mapambano ya magonjwa hayo lakini rai yangu kwa watumishi mara tu itakapokamilika uandaaji wa kadi hii waanze kuitumia kurahisisha utoaji wa huduma na namna ya kukabiliana na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele”amesema.
Kwa upande wake Meneja Mpango wa Taifa wa Magonjwa Yaliyokuwa hayapewi kipaumbele , Wizara ya Afya Dkt.George Kabona ametoa wito kwa jamii kuacha aibu na kujificha pindi wanapokumbwa na magonjwa na badala yake ijitokeze kwa ajili ya kupata matibabu .
“Magonjwa ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele ni magonjwa ambayo jamii yenyewe haitoi kipaumbele na wakati mwingine inawaficha wagonjwa mfano Matende na Mabusha ni watu wenyewe ambao wapo kwenye jamii wakati mwingine wamefichwa au wenyewe wamekata tamaa, lakini kuna magonjwa kama vile ya Vikope ambayo yanaathiri macho hasa tunapofikia utu uzima tunadhani kuwa upofu ni halali yetu ,kumbe magonjwa kama haya yanazuilika kwa kumezesha Kinga Tiba hivyo nawasihi wananchi wanapoona kampeni wajitokeze”amesema.
Pia, amesema kufuatia kuzinduliwa Kituo cha Umahiri masuala ya Afya Kidijitali na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe mafunzo hayo ya kadi ya alama (Score) yanaenda sambamba katika uimarishaji wa kidijitali kukabiliana na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.
Kwa upande wake Mshauri Mwandamizi wa Malaria kutoka Taasisi ya Wakuu wa Nchi za Kiafrika wanaopambana na Malaria(ALMA) ametumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana katika kukabiliana na Magonjwa .
“Niipongeze Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya,Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kuendelea kushirikiana hasa kwa kutumia hii kadi ya alama katika utatuzi wa changamoto kwenye sekta ya afya”amesema.
Ikumbukwe kuwa Kadi ya Alama (Score Card) ni namna ya utoaji wa viashiria mbalimbali kwa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele katika ngazi mbalimbali ikiwemo Vituo vya kutolea Huduma za Afya na kuweza kutatua changamoto na kadi hii hutumia kwa kuangalia rangi na kuweza kutambua eneo fulani lina hali gani ya afya na kuleta suluhisho kwa haraka.