NA DENIS MLOWE, IRINGA
KAIMU Katibu Tawala Msaidizi Viwanda na Bishara, Asifiwe Mwakibete amewataka wasanii wa mkoani Iringa kuichangamkia fursa za mkopo kwa wasanii inayotolewa na Serikali kupitia fedha za Mfuko wa Sanaa.
Akizungumza hivi karibuni alipokuwa mgeni rasmi Katika semina juu ya Mikopo kwa wasanii, Mwakibete alisema kuwa wasanii mkoani hapa wahakikishe wakifanikiwa kupata wanatumia fedha za mfuko huo kuinua sanaa na kazi zao kwa ujumla ziwe kwenye ubora unaotakiwa.
Alisema kuwa kupitia fedha hizo waongeze ubunifu ili kujiweka katika mazingira ya kupata soko la uhakika ndani na nje ya nchi.
Mwakibete amewataka wasanii watakaonufaika na mpango huo kuwa waaminifu katika urejeshaji wa mikopo hiyo ili iweze kuwasaidia wasanii wengine kukopa.
Alimshukuru rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dk. Samia Hassan Suluhu kwa kuwaona wasanii kupitia Mfuko huo kwani utakuwa mkombozi kwao katika kuboresha kazi zao na kukuza kipato wasanii wa mikoani na Tanzania kwa ujumla.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, Nyakaho Mahemba amewataka wasanii wa fani mbalimbali mkoani Iringa kujiandaa kunufaika na mfuko huo kwa kuandaa sanaa zitakazoboresha maslai yao na kukuza uchumi wao.
Alisema kuwa serikali kwa kupitia benki za NBC na CRDB, mfuko huo unatarajia kutoa mikopo mipya ya zaidi ya Sh bilioni 20 kwa wasanii mbalimbali hapa nchini kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 ambapo Hadi sasa Kuna wasanii wameza kunufaika na mkopo huo.
“Serikali ya awamu ya sita kupitia Mfuko wa Sanaa imeamua kutatua changamoto ya wasanii ambayo ni mtaji kwa kuwapatia fursa ya mikopo na elimu ya namna itakayowawezesha kuboresha kazi zao ili mikopo watakayopata iwape tija, na kuboresha Kazi zao za sanaa” Alisema
Mahemba alisema mfuko huo unatoa huduma katika maeneo ya urithi wa utamaduni, lugha na fasihi, sanaa za maonesho, sanaa za ufundi, filamu, muziki na fani nyingine zenye mlengo wa utamaduni na sanaa kwa watu binafsi, vikundi au makundi.
Alisema tangu uzinduliwe Disemba mwaka jana umekwisha wanufaisha wasanii 45 kiasi Cha Sh bilioni 1.077 ambao kati ya wanaume ni 29 waliowezeshwa Sh milioni 737, wanawake 12 Sh milioni 275, kikundi kimoja Sh milioni 10 na makampumi matatu Sh milioni 55.
Aliongeza kuwa miongoni mwa wanufaika mkopo huo ni kundi la walemavu lenye wanachama 22 wanaojishughulisha na uandaaji wa tamthilia, uibuaji wa vipaji vya tasnia kwa walemavu wenzao na watoto.
Naye Meneja wa Bidhaa na Huduma benki NBC kuroka makao makuu, Jonathan Bitababaje alisema benki yao imejipanga vyema kufanikisha mpango huo wa utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa wasanii ambapo wanaanza Mikopo inaanzia Sh 200,000 hadi Sh milioni 100 kwa mkopaji mmoja.
Alisema kuwa wasanii mkoani hapa wanachotakiwa kufanya ni kwenda katika ofisi za utamaduni katika wilaya walipo au mkoa ili wakajiandikishe na kuanza taratibu za kunufaika na mikopo huo wenye riba nafuu kwao.
Na mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Mkoa wa Iringa Hamis Nurdin ameishukuru serikali kwa kuwaletea fursa hiyo akisema watahakikisha wanaitumia ipasavyo ili isaidie kuboresha kazi zao na hatimaye kuwaingiza katika soko la ushindani katika kutengeneza kazi Bora zaidi.
Alisema kuwa awali walikuwa wakiandaa Kazi za Sanaa kwa kiwango hafifu kutokana na ufinyu wa bajeti hivyo kuja kwa fursa hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kufanya filamu zenye ubora tofauti na awali.