Kamishna msaidizi wa magereza mkoa wa Arusha ,ACP Nsajigwa Mwankenja akizungumza kuhusu shughuli mbalimbali za kilimo na ufugaji wanazofanya .
Kamishna msaidizi wa magereza ,ambaye ni Mkuu wa magereza mkoa wa Kilimanjaro ,Leonard Burushi akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha .
Julieth Laizer,Arusha.
Wakulima wametakiwa kuwatumia wataalamu mbalimbali katika kuboresha kilimo chao pamoja na ufugaji ili kujifunza kutoka kwao na kuweza kulima kilimo chenye tija na faida kwa manufaa yao ya baadaye.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Kamishna msaidizi wa magereza mkoa wa Arusha ,ACP Nsajigwa Mwankenja wakati akizungumza na wakulima pamoja na wafugaji waliotembelea vipando vya magereza vilivyopo Njiro jijini Arusha .
Aidha amesema kuwa, magereza wamekuwa wakijikita katika shughuli za kilimo na ufugaji ambapo wamekuwa wakitumia taaluma wao kufundisha wakulima na wafugaji mbalimbali ambao wameweza kujifunza kuhusu kilimo bora na cha kisasa.
“Magereza tumekuwa tukiwaandaa wafungwa waliopo magerezani kwa kuwafundisha maswala mbalimbali ya kilimo pamoja na ufugaji ambapo wengi wao wameweza kupata ujuzi mbalimbali ambao huenda kuutumia pindi wanapomaliza vifungo vyao na kuweza kujiajiri wakiwa wenyewe .”amesema .
Aidh amefafanua zaidi kuwa wamekuwa wakifanya vizuri katika sekta ya kilimo na ufugaji ambapo wamekuwa wakiwavutia wakulima wengi kuweza kufika katika mashamba yao na kujifunza zaidi kuhusu kilimo bora cha kisasa kutoka kwa wataalamu bora waliobobea katika sekta ya kilimo na ufugaji.
“Mwaka huu magereza kanda ya kaskazini tumefanya vizuri sana katika maonyesho ya nanenane ambapo tumeweza kuibuka washindi wa kwanza taasisi za serikali paredi ya Mifugo,ng’ombe wa maziwa,na mshindi wa kwanza taasisi za serikali katika kundi la wakulima na wafugaji “amesema Mwankenja.
Aidha amewataka wakulima pamoja na wafugaji kuwatumia wataalamu hao kuweza kujifunza kilimo bora na cha kisasa na kuweza kuondokana na changamoto mbalimbali kwani kilimo ndio uti wa mgongo wa nchi yetu na ukitumiwa vizuri una manufaa makubwa sana .
Kwa upande wake Kamishna msaidizi wa magereza, na Mkuu wa magereza mkoa wa Kilimanjaro, Leonard Burushi amesema kuwa,shughuli hizo za ujasiriamali wamekuwa wakifanya kwenye vituo vyao na kuwafundisha wafungwa waliopo magerezani ambao kuwawezesha kutumia elimu hiyo pindi wakimaliza vifungo vyao.