Na Alex Sonna _Dodoma
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salamu (DAWASA) imejipanga kuendelea na kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati saba ikiwemo mradi wa ujenzi wa bwawa la Kidunda, mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha maji wa Rufiji na mradi wa maji Kwala.
Hayo yameelezwa leo Agosti 11,2023 jijini Dodoma na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka Hiyo Kiula Kingu wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa Majukumu kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 na kusema Miradi hiyo itakayotekelezwa kwa jumla ya shilingi bilioni 425.9 inalenga katika kuongeza wingi wa maji yanayozalishwa na DAWASA, kuongeza uwezo wa kuhifadhi maji, kuimarisha mfumo wa usambazaji maji na kuimarisha huduma katika maeneo ambayo hayana mtandao hasa yale ya pembezoni.
Aidha, Kingu amebainisha miradi hiyo itasaidia wananchi kupata huduma za usafi wa mazingira kwa gharama nafuu karibu na maeneo wanayoishi na Wakandarasi wanaotekeleza miradi wanaendelea na ujenzi Gharama za miradi hii ni jumla ya shilingi bilioni 25.7 na wanufaika wa miradi hii wanakadiriwa kufikia milioni 1.8.
Hata hivyo katika hatua nyingine amesema Mradi mwingine unaotekelezwa ni wa kujenga mfumo wa kukusanya majitaka na maeneo nufaika ambapo katika awamu hii ni Mbezi beach, Kilongamwima, baadhi ya maeneo ya Kawe na Salasala. Utekelezaji wa mradi umeanza na Wakandarasi wanaendelea na shughuli za maandalizi ya ujenzi.