MKURUGENZI Idara ya Kilimo na Uhakika wa Chakula, Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Hamad Masoud Ali akizungumza na wakilima, wafugaji na wavuvi kwenye ufunguzi wa semina ya kuwajengea uelewa juu ya fursa zinazopatikana kupitia benki ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, hafla hiyo imefanyika Dole.
OFISA Maendeleo ya Biashara Mkuu Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TIDB) kanda ya Zanzibar, Ashura Akim, akizungumza na wavuvi, wafugaji na wakulima kwenye semina ya kuwajengea uwezo iliyofanyika huko Dole wilaya ya Magharibi ‘A’.
…………………
MKURUGENZI Idara ya Kilimo na Uhakika wa Chakula, Hamad Masoud Ali, amesema kuna umuhimu mkubwa kwa wakulima hapa nchini kutumia fursa mbalimbali ikiwemo mikopo, ili kuongeza uzalishaji wa mazao.
Mkurugenzi huyo alieleza hayo, kwenye hafla ya ufunguzi wa semina iliyowashirikisha wakulima, wafugaji na wavuvi, hafla iliyofanyika katika viwanja vya maonesho ya kilimo vilivyopo Dole.
Alisema ili wakulima, wafugaji na wavuvi wapige hatua, lazima wawe na uhakika wa mtaji, ambapo suala hilo hivi sasa limerahisishwa kwani upo uwezekano wa kuchukua mikopo kwenye taasisi za kifedha.
Alieleza kuwa wakulima wengi wa Zanzibar wamejikita kwenye kilimo cha kujikimu kutokana na kutokuwa na mtaji, hivyo uwepo wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo, utawasaidia kuondokana na changamoto wa mitaji.
Alifahamisha kuwa suala jengine muhimu litakalowafanya wakulima, wafugaji na wavuvi wapige hatua na kupata tija zaidi ni kuhakikisha wanakuwa na elimu ya kutosha kwa sekta wanayoifanyiakazi.
“Tunazungumia kupata tija kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi, kwanza lazima muwe na mitaji ya kuendeleza shughuli zenu, lakini muhimu zaidi ni elimu ya kazi unayoifanya”, alisema mkurugenzi huyo.
Akizungumzia kuhusu lengo la semina hiyo, mkurugenzi huyo alisema itawasaidia kutambua fursa mbali mbali zinazopatikana kwenye benki ya Maendeleo ya Kilimo, sambamba na kuongeza elimu.
Nae ofisa maendeleo ya Biashara Mkuu Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kanda ya Zanzibar, Ashura Akim, amesema taasisi hiyo imeanzishwa kwa lengo la kuwapatia wakulima, wavuvi na wafugaji mikopo itakayowatoa katika kilimo cha kujikimu kwenda kwenye kilimo cha biashara.
Nao washiriki wa semina hiyo wameiomba benki ya maendeleo ya kuweka masharti nafuu ya mkopo kwani huko nyuma wakulima wengi walishindwa kupata mkopo kutokana na kutokukidhi masharti.
Walisema kuwa miongoni mwa faida za kuwepo maonesho ni pamoja na wananchi kupata elimu kuhusiana na mambo mbalimbali, hivyo waliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupata fursa kama hizo.
Benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania TADB ni Taasissi inayomilikiwa na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania iliyoanzishwa mwaka 2015 ikiwa na lengo la kuwapatia mikopo wakulima, wavuvi, wafugaji na watu wote wanaojihusisha na kuyaongeza thamamani mazao yanayotokana na kilimo, ufugaji na Uvuvi.