Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amepongeza juhudi zinazofanywa na Taasisi ya Tulia Trust kwa kuwezesha vijana ili kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Waziri Ulega amebainisha hayo jijini Mbeya alipofanya ziara katika banda la taasisi hiyo kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima (Nanenane) yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale, ambapo amesema Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson ambaye ni muasisi wa Tulia Trust amekuwa akifanya jambo jema kwa kushirikiana na serikali kutambua wananchi wa Mkoa wa Mbeya kupitia taasisi hiyo.
Ameongeza kuwa ni mfano mzuri wa kuigwa na kwamba viongozi na jamii kwa ujumla wana wajibu wa kuiga mfano huo kwa kuwawezesha vijana wanaoshiriki katika kazi hiyo nzuri na weledi mkubwa.
Aidha, ameiomba taasisi hiyo kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha inaendelea kuisadia jamii kukabiliana na changamoto mbalimbali hususan zinazowakabili vijana.
Nao baadhi ya vijana ambao wanafanya kazi katika Taasisi ya Tulia Trust wamesema taasisi hiyo imewabadilisha kifikra kupitia maono mbalimbali na kuwainua kiuchumi pamoja na kuwaondoa kwenye makundi ambayo hayana tija kwao na kujiepusha na vitendo hatarishi kwenye maisha yao.