Na. Gideon Gregory, Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ametoa wito kwa serikali, waajiri na mashirika ya kiraia kuendelea kuwasaidia wanawake wanaofanya kazi kwenye sekta rasmi na zisizo rasmi waweze kunyonyesha watoto ipasavyo.
Wito huu umetolewa jijini Dodoma jana katika maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani ambayo huazimishwa kuanzia 1-7 August kila mwaka.
Taarifa ya Mkuu wa Mkoa, iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri alisema kuwa lengo la maadhimisho haya ni kutoa hamasa kwa jamii pamoja na kusisitiza umuhimu wa kulinda, kuimarisha na kuendeleza unyonyeshaji wa maziwa ya mama na kuweka msukumo wa kipekee katika kuunganisha wadau mbalimbali ili kuendana na malengo ya Maeneleo Endelevu (SDGs).
Alisema kuwa uboreshwaji wa hali ya unyonyeshaji utasaidia kuboresha kipato cha familia na usalama wa kazi, ustawi na afya ya wanawake na watoto, kufaidika kwa waajiri pamoja na kuwepo kwa taifa lenye mfumo imara wa kijamii na kiuchumi.
“Jamii inapaswa kuongeza uelewa kuhusu kuwasaidia wanawake waweze kufanya kazi za uzalishaji pamoja na utunzaji wa watoto wao kwa kuelewa namna ya kuoanisha majukumu ya kulea watoto hasa unyonyeshaji pamoja na shughuli za uzaishaji mali” alisema.
Aliongeza kuwa jamii na wadau mbalimbali wanapaswa kuhimiza utoaji wa likizo ya uzazi bila kuathiri malipo na kuweka mazingira wezeshi mahali pa kazi kama nyenzo muhimu za kuwezesha unyonyeshaji wa maziwa ya mama.
Aliitaka jamii na wadau pia kuhamasisha na kutetea utekelezaji wa mikakati inayowezesha waajiri kuwa karibu na familia, walezi au mama wa mtoto na kutoa msukumo katika kurahisisha na kusaidia wanawake walioajiriwa kuendelea kunyonyesha watoto wao.
“Ni lazima jamii ielimishwe kuhusu sheria ya kulinda haki za uzazi kwa wanawake na kuinua kiwango cha kuboresha na kutekeleza sheria nyingine za kitaifa zinazohusiana na suala hili” alisema.
Naye Afisa Lishe wa Jiji la Dodoma Semeni Juma alisema kuwa ili mama afanikishe suala la unyonyeshaji ni lazima kila mmoja kwenye jamii asimame kwenye nafasi yake ili kumpunguzia mama kazi na msongo wa mawazo.
Alisema kuwa mama anapojifungua anapaswa kzingatia mambo kadhaa ikiwemo kumnyonyesha mtoto ndani ya saa moja baada ya kujifungua, kumnyonyesha mtoto titi moja kwa dakika 15-20 pamoja na kuzingatia namna ya kumpakata mtoto wakati wa kumnyonyesha.
“Mama akizingatia mambo haya itamsaidia mtoto kupata virutubisho vyote vinavyotakiwa pamoja na kujenga uhusiano mzuri kati ya mama na mtoto na kujenga upendo pia” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Save the children Bi. Angela Kauleni, alisema kuwa shirika hilo linashirikiana na serikali na wadau wengine kuhakikisha kuwa taifa lenye nguvu na watoto watakaokuwa vijana na kuchangia katika maendeeo ya taifa linajengwa.
“Tunashirikiana na serikali kutoa elimu ya unyonyeshaji hasa kwa wanawake wanaofanya kazi na mabinti wanaojifungua na kuacha kunyonyesha ili kuhakikisha tunajenga kizazi timamu kisichokuwa na udumavu ili kulihakikishia taifa nguvu kazi imara” alisema.