NA DENIS MLOWE, IRINGA
MJUMBE wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa, Dk. Tumaini Msowoya amewataka vijana wa Uvccm wilaya ya Iringa Mjini kujibu hoja kwa hoja juu ya mambo mbalimbali ambayo yamekuwa yakiibuliwa na wapinzani juu ya serikali inayoongozwa na Rais Dr. Samia Suluhu chini ya Chama Cha Mapinduzi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ziara ya Mwenyekiti wa uvccm wilaya ya Iringa Mjini Aizaki Kikoti tukio lilofanyika kwenye kata ya Mtwivila eneo la dodoma road A , Dk. Msowoya alisema kuwa ifike wakati vijana wa Uvccm wajibu hoja kwenye mitandao ambapo wapinzani wamekuwa wakitumia kwa kiasi kikubwa
Alisema kuwa endapo vijana wakitumika vyema kwenye kujibu hoja kwa hoja kwa Yale ambayo yanaendelea kwenye mitandao itakuwa dawa kwa wale wanaopotosha juu ya utendaji kazi wa serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan.
“Tuna viongozi makini wa Uvccm wilaya ya Iringa endapo utaona hoja kwenye mitandao usijibu ili mradi umejibu kikubwa kama huelewi mfate kiongozi wako mshirikishe ili uwe na majibu yaliyosahihi kuliko kukurupuka” Alisema
Dr. Msowoya alisema kuwa ifike wakati vijana wajue kwamba kesho Yao hujengwa na Leo iliyo makini na kuwataka kuwa vijana ambao wajenge Leo ili kesho iwe Bora Kwa manufaa ya nchi na jamii kwa ujumla.
Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Uvccm wilaya ya Iringa ,Aizack Kikoti alisema kuwa ziara itakuwa ya kata kwa kata, mtaa kwa mtaa ikiwa na lengo la kauli mbiu ya “Usimseme mama Samia ni rais mwenye maono” .
Alisema kuwa katika ziara hiyo watakuwa wanamzungumzia mambo ya maendeleo ambayo yamekuwa yakifanywa na Serikali kwani kumekuwa na mambo ambayo hayako sawa kwa baadhi ya watu kupotosha jamii juu ya maendeleo yanayoletwa na serikali.
Alisema kuwa lengo lingine ni kujenga ushirikiano miongoni mwa vijana na jamii kwa ujumla katika kufanya kazi na kuleta maendeleo ya mkoa wa Iringa na nchi kwa ujumla.
“Sisi kama vijana wa Uvccm tupo, hivyo hatuna budi kama vijana kuungana na vijana wengine kwenye kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na wanajambo la kuunga mkono katika kazi zinazofanywa na Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan na ndio watu wa kumzungumzia mazuri yote .” Alisema
Kikoti aliongeza kuwa wako tayari kumlinda rais kumsemea na kukisemea chama kwa wale wote ambao wamekuwa wapotoshaji na kuelezea utelezaji wa ilani ya ccm katika kata zote 18 za mkoa wa Iringa.
Aidha aliwataka vijana kuilinda nchi na viongozi wote kwani suala la vijana kwa sasa wanatakiwa kuelewa bila wao ni sawa na bure hivyo tafsiri kwa vitendo vile ambavyo vinafanywa na rais.
Alisema kwamba vijana wasisubiri mtu kutoka nje aseme kuhusu yanayofanyika na Serikali kama wanaitakia mema nchi
Naye Katibu wa Uvccm wilaya ya Iringa, Hussein A.Kimu aliwataka viongozi kuwatumia vijana kwenye shughuli zao na kuachana na kuwatumia wahuni ambao wamekuwa wakipotosha juu ya serikali Yao.
Aidha alitoa masikitiko makubwa kwa baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakipuuza mwaliko wa Uvccm pindi wanapoalikwa kwenye shughuli za vijana Hali ambayo imekuwa sugu kwa Sasa kwa baadhi ya viongozi wa ngazi za juu.
Katika uzinduzi huo Msowoya alifanikiwa kuchangia kiasi Cha 250,000 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba ya katibu wa Uvccm wilaya ya Iringa ambao vitu mbalimbali vilichangwa na wanachama na madiwani ambapo mnec Salim Abri aliahidi kutoa bati za jengo Zima.