Mgodi wa uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu wa Buzwagi Ndogo uliopo wilaya ya Igunga mkoani Tabora katika kijiji cha Bulangamilwa umefanikiwa kuchangia Mrabaha wa shilingi 383,821,051.17 kwa kipindi cha miezi mitano kuanzia mwezi Februari mpaka Julai 2023.
Hayo yamebainishwa Agosti 4, 2023 wilayani Igunga Mkoani Tabora na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko alipotembelea na kukagua maeneo mbalimbali za machimbo katika mgodi huo.
Mapema baada ya ukaguzi wa mgodi Dkt.Biteko amezungumza na wachimbaji wanaochimba katika mgodi huo kwa lengo la kusikiliza changamoto mbalimbali zilizopo katika mgodi huo.
Katika mkutano huo Dkt.Biteko alitoa maelekezo mbalimbali kwa uongozi wa mgodi ikiwa ni pamoja na kuondoa tozo ndogo ndogo ndani ya mgodi huo zinazotozwa kwa wachimbaji wadogo kutoka katika masalia ya uchenjuaji madini kama vile mawe ,felo na kwale.
Aidha, Dkt.Biteko amewasihi wachimbaji kufanya uchimbaji kwa kufuata Kanuni , Taratibu na Sheria zinavyoelekeza ikiwa pamoja na kuachana na mawazo ya utoroshaji wa madini
Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mgodi huo Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tabora Mhandisi Abel Madaha alieleza kuwa maeneo mengi ya kijiji cha Bulangamilwa yanayofanyiwa uchimbaji bado hayajakuwa na uzalishaji wenye tija ukilinganishwa na uzalishaji ambao umepatikana katika mgodi huu wa Buzwagi.
Mhandisi Madaha amefafanua kuwa kabla ya mgodi huu kuwa na uzalishaji wenye tija eneo hili lilikuwa na idadi ya leseni za uchimbaji mdogo zisizozidi ishirini ambapo kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji maombi ya leseni yameongezeka kufikia leseni hamsini ambazo tayari zimeishatolewa.
Akielezea juu ya maendeleo ya mgodi huo Mhandisi Madaha alifafanua kuwa wilaya ya Igunga ni wilaya inayoongoza kwa shughuli za uzalishaji wa madini ya Dhahabu katika maeneo ya Igurubi, Matinje, Ntobo, Buchengele na Imalilo na kuifanya wilaya ya Igunga kuwa mojawapo ya wilaya inayochangia zaidi kwenye mapato ya serikali yatokanayo na rasilimali madini mkoani Tabora.