Wenyeviti wa vyama vya ushirika vya msingi(Amcos)wilayani Tunduru wakimsikiliza Mkuu wa wilaya hiyo Wakili Julius Mtatiro(hayupo pichani)kwenye kikao kazi kwa ajili ya maandalizi ya ukusanyaji na uuzaji wa zao la mbaazi kwa msimu 2023/2024.
Makamu mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wilayani TUnduru(Tamcu Ltd)Chipo Chiko Chipojola akifungua kikao kazi cha maandalizi ya ukusanyaji na uuzaji wa zao la mbaazi kilichofanyika katika ukumbi wa Klasta ya walimu mjini Tundutu,katikati Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro.
Meneja masoko wa Chama kikuu cha Ushirika wilayani Tunduru(Tamcu Ltd) Marcelino Mrope akitoa taarifa ya ukusanyaji wa zao la mbaazi kwa msimu 2022/2023 kwenye kikao cha maandalizi ya msimu mpya 2023/2024 kilichoongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro.
Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru(Tamcu)Imani Kalembo akitoa ufafanuzi wa mfumo utakaotumika kwenye ununuzi wa zao la mbaazi kwa msimu 2023/2024 kwenye kikao kazi kilichowakutanisha mameneja wa vyama vya msingi vya ushirika,wenyeviti na maafisa ushirika wa wilaya hiyo,katikati makamu mwenyekiti wa Tamcu Pino Chipojola na kulia Mkuu wa wilaya Julius Mtatiro.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiro,akizungumza na mameneja na wenyeviti wa vyama vya msingi vya ushirika(Amcos),maafisa tarafa na viongozi wa chama kikuu cha Ushirika Tamcu Ltd kwenye kikao kazi cha maandalizi ya ununuzi na ukusanyaji wa zao la mbaazi kilichofanyika katika ukumbi wa Klasta mjini Tunduru,
Baadhi ya wenyeviti wa vyama vya msingi vya ushirika wilayani Tunduru wakipitia taarifa za hali ya uzalishaji wa zao la mbaazi katika msimu wa kilimo 2022/2023 na malengo ya uzalishaji kwa msimu 2023/2024.
Na Muhidin Amri,
Tunduru
MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro,amewaagiza viongozi wa vyama vya msingi vya Ushirika(Amcos)na idara ya Ushirika Halmashauri ya wilaya Tunduru kuhakikisha wanadhibiti utoroshaji wa zao la mbaazi na kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuwasaidia wakulima waweze kujiinua kiuchumi.
Mtatiro amesema hayo jana, wakati akizungumza na mameneja na wenyeviti wa Amcos,maafisa tarafa na viongozi wa Chama kikuu cha Ushirika(Tamcu katika kikao cha maandalizi ya makusanyo ya zao hilo na mazao mchanganyiko kwa msimu wa masoko 2023/2024.
“mwaka jana kulikuwa na ucheleweshaji kutokana na watu wa mifumo kuchelewa kufanya uzembe hali iliyopelekea kuchelewa kuanza msimu wa makusanyo na ununuzi wa mbaazi,mwaka huu sitaki kusikia hali hiyo inajitokeza tena”alisema.
Aidha alisema,zao mbaazi katika msimu 2023/2024 litaendelea kuuzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na kuwaonya wakulima,viongozi,watunza maghala na wanunuzi wanaokusudia kuharibu mfumo huo ambao umeonyesha mafanikio makubwa kwa wakulima.
Amewataka viongozi wa vyama na bodi za Ushirika wilayani humo,kuwa waaminifu na kuepuka kujihusisha na ubadhirifu,bali wahakikishe wanaongoza vyama hivyo kwa kufuata taratibu na sheria za vyama vya Ushirika.
“hakutakuwa na huruma kwa yoyote atakayejaribu kuvuruga ununuzi wa mbaazi katika msimu wa mwaka huu,nawaombeni sana viongozi wenzangu twendeni tukawasaidia wakulima wetu huko vijijini”alisisitiza Mtatiro.
Amewataka wakulima,kutokubali kudanganywa na wafanyabiashara wanaopita kwenye maeneo yao kwa ajili ya kuhitaji kununua mbaazi nje ya mfumo huo kwa bei ndogo isiyolingana na gharama za uzalishaji na kueleza kuwa,serikali imejipanga kuwashughulikia watu hao.
Alisema,mfumo wa soko huria ni wa kinyonyaji na hauna nafasi tena katika wilaya hiyo kwa kuwa ndiyo uliosababisha wakulima wa mikoa ya kusini kuendelea kuwa maskini kwa muda mrefu licha ya jitihada kubwa wanazofanya mwaka hadi mwaka.
Alisema,dhamira ya serikali ni kuona sekta ya kilimo inawanufaisha wakulima kwa kupata fedha zinazostahili na serikali inapata ushuru ambao utakwenda kutumika kuharakisha maendeleo na kuboresha huduma muhimu za kijamii.
Mtatiro,amewaasa viongozi na watendaji wa sekta ya ushirika kuhakikisha wanakutana na wakulima ili kuwaeleza faida za ushirika na maafisa ugani kuwatembelea kwenye shughuli zao mara kwa mara ili kuwapa ushauri wa kilimo cha kisasa na chenye tija kwa kuwa wakulima wakisimamiwa vizuri watazalisha kwa wingi na Amcos zitapiga hatua kubwa ya kiuchumi.
Afisa ushirika wa wilaya hiyo George Bisan alisema,msimu wa mwaka 2020/2021 na 2021/2022 changamoto kubwa ilikuwa utoroshaji wa zao la mbaazi kwenye vijiji vinavyopakana na mikoa jirani ambayo hakuwa mfumo huo.
Kwa upande wake Meneja mkuu wa Tamcu Iman Kalembo alieleza kuwa, katika msimu 2022/2023 Chama kikuu kwa kushirikiana na vyama vya Ushirika vya msingi viliweka malengo ya kukusanya kilo milioni 5,451,000.
Hata hivyo alisema kuwa,kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao walifanikiwa kukusanya kilo milioni 3,035,692 ambazo ni pungufu kwa kilo milioni 2,415,308 sawa na anguko la asilimia 44.31 ya lengo.
Kalembo alieleza kuwa,mbaazi ziliuzwa kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani na jumla ya minada sita ya mauzo ilifanyika ambapo bei ya wastani ilikuwa Sh. 898.25 na jumla ya kilo 3,035,692 ziliuzwa zenye thamani ya Sh.bilioni 2,633,233,690.00.
Naye meneja masoko wa Tamcu Marcelino Mrope alisema, katika msimu wa mwaka huu Chama kikuu kupitia vyama vya ushirika vya msingi,kimeweka malengo ya kukusanya mbaazi kilo milioni 5,350,788.