Na Mwandishi wetu, Simanjiro
DIWANI wa Kata ya Edonyongijape Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Jacob Kimeso amechaguliwa kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kupitia CCM.
Katika uchaguzi huo uliokuwa na wagombea saba, Kimeso ambaye ni Makamu Mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa mwaka mmoja ameshinda kuwa mgombea kwa kupata kura 16.
Kimeso akizungumza baada ya kuchaguliwa kugombea nafasi hiyo ya mwaka mmoja, amewashukuru madiwani hao kwa kuwa na imani naye hadi kumrudishia tena umakamu mwenyekiti.
Amesema imani huzaa imani, amewaahidi kuendelea kutumikia nafasi hiyo ya kumsaidia Mwenyekiti, kwa lengo la kufanikisha maendeleo ya wilaya ya Simanjiro yenye neema tele.
“Ndugu zangu wahehimiwa madiwani nachukua nafasi hii kuwashukuru kwa kunichagua tena kwa mara ya pili kwa nafasi ya makamu mwenyekiti wa halmashauri nawaahidi sitawangusha tuko pamoja kazi iendelee,” amesema Kimeso.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ambaye ndiye amesimamia uchaguzi huo amewataka madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kuachana na makundi ya kisiasa, wajikite kupambania maendeleo ya watu waliowachgua.
Sendiga amesema madiwani wote wa Simanjiro wanatokea CCM, hivyo wahakikishe wanaondokana na makundi ya uchaguzi na kujikita kwenye suala la maendeleo.
“Uchaguzi tuu wa kumpata mgombea wa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri kupitia CCM umechukua siku nyingi kufanyika, sababu ya malumbano, sasa leo umefanyika acheni migogoro fanyeni kazi,” amesema Sendiga.
Amesema anatarajia baada ya uchaguzi huo kumalizika Simanjiro, kitakachofuata ni umoja na maendeleo na siyo kuendeleza malumbano na migogoro isiyo na tija.
“Wote mmechaguliwa kwa ajili ya kufanikisha maendeleo ya wapiga kura wenu, hivyo sitarajii kuona tena mnaendeleza malumbano badala ya kusimamia miradi ya elimu, afya, maji, miundombinu na mengineyo,” amesema Sendiga.