* Wananchi wengi wasusia mikutano yake kwa unafiki wake kwa Magufuli
Na Mwandishi Wetu, Geita
MAKAMU Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, amezomewa na wananchi wa kanda ya ziwa katika mikutano ya hadhara ya chama hicho cha upinzani, huku wakimshutumu kwa unafiki anaouonesha kwa aliyekuwa Rais John Magufuli.
Video na picha kutoka kwenye mikutano ya hadhara ya Lissu kanda ya ziwa ambazo zimesambaa kwenye mitandao ya jamii zinaonesha akiwa anazomewa na wananchi, huku watu wachache wakihudhuria mikutano hiyo.
Viongozi wa CHADEMA, wakiongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu John Heche kutoka mkoa wa Mara, wamekuwa wanamnadi Lissu kama “Rais” kwenye mikutano yake, licha ya mchakato ya kumpata mgombea urais wa chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao wa 2025 kuwa bado haujafanyika.
Heche na viongozi wengine wa CHADEMA wameingiwa na fedheha kubwa kutokana na Lissu kuzomewa na kususiwa na wananchi wa kanda ya ziwa katika mikutano inayoendelea.
Wananchi hao wameonesha kutomkubali Lissu kutokana na kugeugeu au unafiki anaouonesha kwa hayati Rais Magufuli, ambaye alikuwa na wafuasi wengi kanda ya ziwa.
Akiwa Biharamulo, Lissu alipata wananchi wachache katika mkutano wake na walianza kumzomea alipoanza kuongelea mambo ya bandari ya Dar es Salaam.
Hali hiyo ilimfanya Lissu kuonesha hulka yake ya kutopenda kukosolewa kwa kutaka watu wanaomzomea waondolewe mara moja kwenye mkutano huo.
“Kama kuna mtu anataka kuleta kelele na hawezi kutulia, nawaombeni muwaondoe kimya kimya,” alisema Lissu akiwa jukwaani baada ya kuzomewa na wakazi wa Biharamulo kwenye mkutano wake wa hadhara juzi.
Kitendo cha Lissu kuzomewa na wananchi wa kanda ya ziwa na mikutano yake kukosa mvuto na kuhudhuriwa na watu wachache ni ishara kuwa amekosa ufuasi kwenye kanda hiyo muhimu katika siasa za Tanzania.
“Sisi wananchi wa kanda ya ziwa kamwe hatutasahau maneno ya kejeli ya Lissu dhidi ya Rais Magufuli kwa kusema kuwa kifo chake kimeleta ahueni kwa taifa. Leo Lissu huyo huyo anageuka na kusema eti anataka aende Chato kumuombea Magufuli kwenye kaburi lake. Kwani anatuchukuliaje sisi wananchi?” Alihoji Simon Simba, mkazi wa mkoa wa Geita.
Lissu akiwa anaishi uhamishoni nchini Ubelgiji alikuwa akitoa lawama moja kwa moja kwa Rais Magufuli baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana jijini Dodoma mwaka 2017 na kusema kuwa amefurahia kifo cha Maguufuli.
Lissu aliwahi kusema hadharani mara kadhaa kuwa kamwe hawezi kutembelea kaburi la Magufuli, Chato, kwa kuwa aliwatesa wapinzani na alimlaumu kuhusika na jaribio la kutaka kumuuwa.
Mwanasiasa huyo wa upinzani alienda mbali kwa kudai kuwa kifo cha Magufuli kimeleta “ahueni” kwa taifa.
Kwa sababu za kisiasa, Lissu amekuwa akijaribu kuwachochea wananchi dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya upotoshaji kuwa Rais ameuza nchi na kudai kuwa sasa yeye Lissu anamkumbuka Magufuli kwa mema.
Katika hali ya kushangaza, baada ya mjadala wa DP World kuibuka, Lissu amedai kuwa ataenda kwenye kaburi la Magufuli kumuombea na anatamani afufuke.
Kauli hizo za kutatanisha za Lissu zimeonesha kuwakera wakazi wengi wa kanda ya ziwa ambao wamesusia mikutano yake na kumzomea na kufanya ziara yake ipooze kwa kuhudhuriwa na watu wachache.