Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa sugu watano wanaotuhumiwa kujihusisha na makosa ya kughushi vyeti vya udereva vinavyotolewa na chuo cha Veta na leseni za udereva. Pia, wengine Wawili kwa kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu/utapeli wakituma jumbe fupi kwa watu mbalimbali ‘’tuma kwenye namba hii’’
Awali, tulipata taarifa kutoka kwa raia wema juu ya uwepo wa wahalifu hao ambapo askari Polisi walifanya ufuatiliaji wa haraka na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao kwa wakati tofauti ambapo Julai 25, 2023 alikamatwa Esau yakobo, miaka 26, mkazi wa Mecco kaskazini, Wilaya ya Ilemela kwa kosa la kughushi vyeti na leseni za udereva akiwa na vyeti vyenye majina na namba, vivuli mbalimbali vya leseni za udereva, picha mbalimbali za “Passport size”, barua mbalimbali za Polisi ambazo zimeghushiwa saini ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza.
Aidha, mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya kukamatwa kwa John Msemo, miaka 45, afisa mauzo wa Kampuni ya Chrolide exide aliyefika kituo cha Polisi kwa ajili ya uhakiki wa madaraja ya leseni yake akiwa na barua iliyoghushiwa saini ya Julai 5, 2023 iliyohusu uhakiki wa leseni ya udereva pamoja na cheti cha udereva alivyodai kuvipata kutoka kwa Sixmond George, miaka 48, mkufunzi wa chuo cha udereva Nyanza na mkazi wa Igoma baada ya kumpatia pesa.
Mtuhumiwa mwingine aliyekamatwa ni Samwal Bose, miaka 47, mwalimu wa chuo cha udereva Chanila na mkazi wa Ibanda juu ambaye amekutwa na barua ya kughushi iliyohusu uhakiki wa leseni
1 | P a g e
kutoka Jeshi la Polisi ambazo wamekuwa wakizitumia kujinufaisha kwa kuwaadaa wananchi na kuwatengenezea vyeti batili. Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata mtandao wa wahalifu hao na vifaa walivyokuwa wakivitumia kughushi nyaraka hizo ikiwemo Printer moja aina ya Epson, Computer moja aina ya HP na Flash Mbili. Watuhumiwa wote wamehojiwa kwa kina na watafikishwa Mahakamani baada ya kukamilishwa kwa upelelezi.
Pia, tarehe 27 Julai, 2023 majira ya 07:00 asubuhi huko katika bandari ya kaskazini, Jijini Mwanza askari Polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili, Abdulahim Karungila, miaka 41, mkazi wa mtaa wa Rwazi, Kata ya Kahororo, Bukoba mjini na Heri kabuya, miaka 36, mkazi wa mtaa wa kyaya, Kata ya Kahororo kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya uhalifu mitandaoni.
Watuhumiwa hao wamekutwa wakiwa na nyaraka za watumishi na wastaafu wa Serikali zikiwa katika mfumo wa machapisho mbalimbali pamoja na line mbalimbali za simu. Baada ya mahojiano ya kina, watuhumiwa wamekiri kujihusisha na vitendo vya uhalifu mitandaoni na kwamba matukio hayo ya kuwapigia simu watumishi wa serikali na kuwatajia kumbukumbu zao za daftari la utumishi huku wakiwataka watume pesa ili wawarekebishie kumbukumbu zao za utumishi. Hata hivyo, Jeshi la Polisi limebaini kuwa watuhumiwa hao wamekuwa wakifanya uhalifu huo katika Mikoa ya Kagera, Mwanza na Dar es salaam.
Katika tukio linguine, tarehe 25.07.2023 muda wa saa 19:30 usiku katika kijiji cha Ntundu, Kata ya Busangi, Wilaya ya Msalala, Mkoa wa Shinyanga askari walifanikiwa kumkamata Prisca Clement, miaka 25, mkazi wa Buhingo, Wilaya ya Misungwi kwa tuhuma za kuiba mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi 9
Mtoto huyo aliibiwa tarehe 10.07.2023 visiwani Zanzibar baada ya mzazi wa mtoto huyo kumuachia Prisca Clement amuangalie wakati alipokuwa kwenye majukumu mengine ndipo mtuhumiwa alipata nafasi ya kutoroka na mtoto huyo mpaka Mkoa wa Mwanza na baadaye Mkoa wa Shinyanga
alipo kamatiwa.
Baada ya kumuiba mtoto huyo mtuhumiwa alienda kumficha kwa mama yake mzazi aitwaye Maria Furaha mkazi wa kijiji cha Buhingo kata ya Inonelwa Wilayani Misungwi ambapo mtoto huyo alipatikana na kutambuliwa kuwa ndiye aliyeibiwa visiwani Zanzibar. Baada ya mahojiano
mtuhumiwa amekiri kuhusika na wizi wa mtoto huyo kwa lengo la kwenda kumuuza.
Jeshi la Polisi lilipata taarifa kutoka kwa wazazi wa mtoto huyo kuwa mtoto wao ameibiwa na mtuhumiwa amekimbilia Mikoa ya kanda ya ziwa. Ufuatiliaji wa haraka ulianza mara moja na kufanikiwa kumpata mtoto huyo aliyekuwa ameibiwa akiwa salama. Aidha, Tumefanya mawasiliano na wazazi wa mtoto huyo na atakabidhiwa kwao baada ya kukamilisha taratibu za kisheria na Mtuhumiwa atafikishwa Zanzibar kukabilana na kesi yake.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linaendelea kutoa wito kwa wakazi wote wa Mkoa wa Mwanza hususani watumishi na wastaafu kuwa makini na kufuata njia sahihi za kutatua changamoto za kiutumishi zinazowakabili kwa kufika katika Idara husika ili kutatua changamoto hizo. Aidha, tunatoa ushauri kwa wananchi wote kutofuata maelekezo kutoka kwenye namba wasizozifahamu zikiwataka kutoa taarifa zao kwa watu wasiowafahamu au kuwatumia fedha. Pia, wazazi na walezi kuongeza umakini katika uangalizi wa watoto wao na sio kumuamini kila mtu na kumwachia mtoto.
Imetolewa na;-
Wilbrod W. Mutafungwa- SACP
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza