St. Petersburg – Urusi
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amemwakilisha Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Serikali ya Urusi na nchi za Afrika uliaonza tarehe 27 hadi 29 Julai, 2023 katika jiji la St. Petersburg nchini Urusi.
Mkutano huo unalenga kukuza na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi ya Urusi na nchi za Afrika hususan katika Sekta ya Madini, uchumi, kukuza teknolojia na masuala mengine ya kiuchumi ikiwemo sekta ya ujenzi na uchukuzi, kilimo, utamaduni, nishati, uchumi wa bluu.
Katika mkutano huo, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko alishiriki katika mijadala mbalimbali na kuwasilisha masuala muhimu yanayohusu Sekta ya Madini.
Dkt. Biteko aliwaeleza washiriki wa mkutano huo kuhusu fursa zilizopo katika Sekta ya Madini ili kuvutia uwekezaji. Aliyataja baadhi ya maeneo kuwa ni pamoja na shughuli za utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji, uongezaji thamani madini na biashara ya madini nchini.
Washiriki wengine katika mkutano huo ni pamoja na Wafanyabiashara na watu mashuhuri kutoka nchi ya Urusi na nchi za Afrika. Mkutano wa kwanza wa aina hii ulifanyika Oktoba 23 na 24 2019 katika mji wa Sochi nchini Urusi.