Maonesho ya wakulima ya Nanenane Kimataifa yanatarajia kufanyika mkoani Mbeya ambapo taasisi, mashirika ya serikali, mashirika binafsi na watu binafsi watashiriki katika maonesho hayo. Aidha, mataifa zaidi ya 30 yanatarajia kushiriki maonesho hayo yatakayofanyika katika uwanja wa John Mwakangale Jijini Mbeya mapema mwishoni mwa mwezi Julai, 2023.
Kwa kutambua ukubwa wa maonesho na sherehe za Nanenane Kimataifa Mkoani Mbeya, wageni wa kitaifa na kimataifa, mataifa washiriki na wageni kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania bara na visiwa ambao watafika kushiriki au kutembelea viwanja vya maonesho hayo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga vizuri kuimarisha ulinzi na usalama muda wote wa maonesho hayo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lipo imara kuwahakikisha wageni wote usalama wao na mali zao kwa kuhakikisha ulinzi unaimarishwa maeneo yote ya uwanja, ndani na nje kwa kushirikiana na Jeshi la Akiba, SUMA JKT na Walinzi wa Makampuni binafsi ya ulinzi.
Aidha, kutokana na changamoto ya miundombinu ya Barabara hasa maeneo ya Mafiati, Mwanjelwa, Kabwe, Soweto hadi Nanenane, tunawataka watumiaji wote wa barabara kuwa wavumilivu na kuheshimu sheria za usalama barabarani. Jeshi la Polisi litakuwepo muda wote maeneo hayo kwa ajili ya kuongoza magari na watumiaji wengine wa barabara ili kupunguza msongamano.
Sambamba na hayo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawakumbusha wamiliki wa nyumba za kulala wageni na kumbi za starehe kuhakikisha wanaweka walinzi binafsi walioajiriwa na makampuni binafsi ya ulinzi yanayotambulika ili kuimarisha ulinzi katika maeneo yao ambayo tunatarajia wageni kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi watafikia.
Jeshi la Polisi litaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali kwa kufanya doria za magari, pikipiki, miguu na kwa kutumia Mbwa wa Polisi, pia watendaji wa Kata na Mitaa ambao ni walinzi wa amani katika maeneo yao, kuhakikisha vikundi vya ulinzi shirikishi vinafanya kazi kwa kushirikiana na wakaguzi wa Kata na Polisi Kata ili kuzuia na kudhibiti uhalifu.
Kauli mbiu ya Maonesho ya Nanenane 2023 Kitaifa Mkoani Mbeya ni “Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula”
Imetolewa na:
BENJAMIN KUZAGA
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.