Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa Deogratias Ndejembi akimzungumza na wananchi wa Kata ya Lilambo Manispaa ya Songea
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Lilambo Manispaa ya Songea wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa Deogratias Ndemjembi
Na Albano Midelo,Songea
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa Deogratias Ndejembi amesema serikali ya Awamu ya sita mwaka huu imetoa zaidi ya shilingi bilioni 230 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi nchini.
Akizungumza na wananchi wa wilaya za Songea,Mbinga na Nyasa kwa nyakati tofauti amesema katika Mkoa wa Ruvuma serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 7.7 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi shule mpya za msingi kupitia program ya (BOOST).
Amesema serikali pia katika mwaka 2022/2023 imetoa zaidi ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za sekondari 176 za kata kupitia program ya SEUIP.
“Fedha hizo zimetolewa kujenga shule za sekondari za kata katika kata zisizo na shule na kata zenye wanafunzi wengi zaidi ukilinganisha na miundombinu ya shule zilizopo’’,alisema Ndemjembi.
Hata hivyo amesema katika Mkoa wa Ruvuma kupitia program hiyo,serikali imetoa shilingi bilioni 3.9 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya saba za sekondari za kata.
Kwa upande wake Mbunge wa Songea mjini na Waziri wa Sheria na Katibu Dkt.Damas Ndumbaro akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha nyingi zinazotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa vyumba vingi vya madarasa vilivyopunguza msongamano wa wanafunzi darasani.
Amesema serikali imejenga shule mpya za msingi na sekondari Pamoja na kujenga maabara za kisanyansi kwa ajili ya shule za sekondari na kwamba mwaka huu serikali imetoa fedha za kuanza ujenzi wa chuo kikuu cha serikali katika eneo la Pambazuko Kata ya Tanga.
Mkoa wa Ruvuma una jumla ya shule za msingi 841 na shule za sekondari 233.