Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba amesema kuwa mwisho wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Mtaji Rasilimali Watu mnamo Julai 26, 2023, Afrika inategemea uwekezaji mahususi utakubalika na kwamba Rasilimali Watu Itapewa kipaumbele.
Katibu Mkuu, Dkt. Natu ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akihojiwa mubashara na kituo cha Redio cha East Africa kijulikanacho kama “Supa Breakfast” kuhusu ujio wa mkutano mkubwa wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Mtaji Rasilimali Watu utakaofanyika jijini Dar es Salaam Julai 25 na 26, 2023.
Amefafanua kuwa, mkutano huo umewakutanisha viongozi wa mataifa ya Afrika ili waweze kuzungumza namna ya kuwekeza kwenye bara la Afrika ambapo idadi ya watu barani humo imefikia takriban bilioni 1.2 huku karibu asilimia 60 ni vijana chini ya miaka 25 ambapo takwimu hizo zinamaanisha kuwa ni lazima Afrika iwekeze kwenye rasilimali watu kwa kuwa na sera za makusudi na uwekezaji ambao unawalenga vijana ili kuwa na nguvu kazi ambayo itajenga nchi zetu.
“Mategemeo ni kwamba lile Azimio la Dar es Salaam kuhusu Rasilimali Watu litakuja kwa namna ya kuwa sisi nchi za Afrika lazima tushirikiane kikanda kwenye suala la uwekezaji kwa vijana, kila nchi ijiwekee malengo na malengo hayo yafikiwe na rasilimali watu iwe sekta ya kipaumbele,” alisema Dkt. Natu
Ameeleza kuwa, pamoja na kwamba teknolojia ni muhimu na itatumika sana lakini rasilimali watu bado inahitajika na itatumika kwani nia na madhumuni ni kuoanisha teknolojia na ajira kwa vijana.
Akieleza kwa upande wa Tanzania, Dkt. Natu amesema kuwa, ifikapo mwaka 2050, kutakuwa na asilimia 70 ya vijana chini ya miaka 30, hivyo ni lazima kuwekeza sasa kwani bila kufanya hivyo, wakati ukifika kutakuwa na changamoto kubwa.
Amewataka vijana wajue kwamba viongozi wa Serikali waliokutana katika mkutano huo wana nia ya kuwaingiza katika mkondo wa kufanya kazi kwa tija.
Mpaka sasa, viongozi wa kitaifa 30 wamethibitisha kushiriki, baadhi kwa kuja wenyewe na wengine kupitia uwakilishi, mkutano huu utahudhuriwa na Marais, Makamu Marais, Mawaziri Wakuu, Manaibu Waziri Wakuu. Mawaziri na Mabalozi.
Vilevile kuna uthibitisho wa mawaziri 80 ambao watajumuika katika mkutano huu, washiriki wengine ni kutoka Mashirika ya Kimataifa ya fedha, Taasisi za Elimu na Asasi za Kiraia.
[20:22, 24/07/2023] Jack H: Utazituma tu muda wowote hata kama ni usiku…naomba nisaidie itume kila moja kivyake.