Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi (aliyeketi katikati) akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yaliyobainishwa katika taarifa ya Mkoa ya utekelezaji ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Salha Burian (wa kwanza kushoto), wa kwanza kulia ni Katibu wa CCM Mkoa wa Tabora Elias Mpanda na wa pili kushoto ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (MNEC) Mohamed Nassoro Hamdan (MEDDY) Lucas Raphael,
Na Lucas Raphael,Tabora
SERIKALI ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetenga kiasi cha sh bil18.4 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere cha Kilimo na Biashara Kampasi ya Tabora.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kwa kipindi cha miezi 6, Januari-Juni 2023 katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM.
Alisema ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 imetoa mwongozo juu ya utolewaji elimu ya juu katika maeneo mbalimbali ya kimkakati ili kupanua wigo wa fursa za vijana kujiajiri.
Alibainisha kuwa serikali imewaletea mradi wa ujenzi wa Shule Kuu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Biashara ya Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere itakayojengwa katika kata ya Itonjanda, halmashauri ya manispaa Tabora.
Balozi Batilda alifafanua kuwa manispaa hiyo tayari imetoa eneo lenye ukubwa wa ekari 158 kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho utakaogharimu kiasi cha sh bil 18.4 hadi kukamilika kwake.
‘Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutuletea mradi wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere -Shule Kuu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Biashara, hii ni fursa muhimu sana kwa Mkoa wetu’, alisema.
Balozi Batilda alisema kwamba mkoa umeendelea kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa bidii na mafanikio makubwa katika sekta zote ikiwemo elimu, miundombinu ya barabara, maji, uwezeshaji wananchi kiuchumi na ujenzi miundombinu ya barabara na reli.
Alisema kuwa Mipango mingine ni ujenzi wa bandari kavu na usambazaji umeme wa REA katika vijiji vyote vya Mkoa huo ambapo hadi sasa vijiji 606 vimefikiwa na nishati hiyo na vijiji 119 vilivyobakia vitapata huduma hiyo kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Sekta nyingine ambazo miradi imeendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa ni maji, kilimo na ushirika, mifugo na uvuvi, misitu , uhifadhi na uzalishaji mazao ya misitu, ufugaji nyuki na uchakataji mazao yake na michezo na utamaduni.
Aidha katika kupanua wigo wa fursa za ajira kwa vijana wa Mkoa huo kupitia Mafunzo ya Ufundi Stadi, RC alisema serikali imetoa kiasi cha sh bil 5.36 kwa ajili ya ujenzi wa Vyuo 2 vya VETA katika wilaya za Uyui na Igunga.
Alibainisha kuwa ujenzi wa vyuo hivyo upo katika hatua za mwisho ambapo Chuo cha Uyui hadi sasa kimegharimu kiasi cha sh bil 2.75 na cha Igunga sh bil 2.61, na kiasi cha sh mil 393.1 kimeongezwa kwa ajili ya kukamilisha Chuo cha Uyui.
Kuhusu sekta ya afya na elimu, RC aliishukuru serikali kwa kuwapatia kiasi cha sh bil 6.85 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba, kukamilisha maboma ya zahanati 19 na kuendeleza ujenzi wa hospitali 3 za wilaya ya Tabora mjini, Urambo na Nzega.
Aidha alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapatia kiasi cha sh bil 12 kwa ajili ya ujenzi wa shule 17 za msingi, vyumba 118 vya madarasa, vyumba 16 vya madarasa ya elimu ya awali, matundu 130 ya vyoo na nyumba 2 za walimu.
Miradi mingine ni ujenzi wa vyumba 565 vya madarasa ya sekondari kwa sh bil 11.3, mingine ni sh bil 4.95 za ujenzi wa madarasi 52, mabweni 25 na matundu ya vyoo 90, na bil 2.19 za ujenzi wa vyumba 33, mabweni 9 na matundu 50 ya vyoo.
Mingine ni sh bil 3 za ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya wasichana Kaliua, bil 8.7 za ujenzi wa sekondari mpya 12, mabweni 2 na nyumba 11 za walimu na bil 2.39 kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo 2.180.