Na Dotto Mwaibale, Singida
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo kesho Julai 23, 2023 anatarajia
kuwasha moto katika mkutano wa hadhara ataoufanya Uwanja wa Bombadia mjini hapa
ambapo atawahutubia maelfu ya wananchi wa Mikoa ya Singida, Tabora na Dodoma.
Katika mkutano huo ambao ataambatana na viongozi wengine waandamizi wa
chama hicho, ajenda kubwa itakuwa kuhusu mkataba wa uwekezaji wa Bandari ya Dar es
Salaam dhidi ya Kampuni ya Dubai Port World (DP World)
Chongolo na viongozi wenzake wanatoa
ufafanuzi kuhusu mkataba huo kwa wananchi wa mikoa mbalimbali baada ya kuwepo
na upotoshaji wa makusudi unaofanywa na baadhi ya watu wanaodai kuwa Serikali
ya CCM imeingia katika mkataba huo ambao hautakuwa na manufaa kwa nchi.
Chongolo na timu yake tayari amekwishafanya mikutano katika mikoa ya Nyanda
za Juu Kusini, Kanda ya Kaskazini, Mikoa ya Kusini na sasa ni zamu ya mikoa ya
Kanda ya Kati.
Mikutano yake yote alioifanya katika mikoa hiyo, Chongolo amekuwa
akisisitiza kuwa suala la uboreshaji wa bandari sio jambo geni bali lipo katika
ilani ya uchaguzi wa CCM ya 2020-2025 chini ya Serikali inayoongozwa na chama hicho.
Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Singida, Ahmed Kaburu akizungumza na
waandishi wa habari jana alisema maandalizi ya mkutano huo yamekamilika kwa asilimia
100 ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wote wa Mkoa wa Singida
kufika kwenye viwanja hivyo kuanzia saa 2:30 asubuhi kwenda kuwasikiliza
viongozi hao wa chama hicho kitaifa.
“Maandalizi yote ya mkutano wetu yapo tayari nitumie fursa hii kuwaalika
wananchi wote kufika kwenye mkutano huu mkubwa ambao utaambatana na burudani za
aina mbalimbali kutoka kwa wasanii wa hapa Singida na nje,” alisema Kaburu.