Naibu Katibu Mkuu Sekta ya Ujenzi, Ludovick Nduhiye akizungumza na Watumishi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RfB) (hawapo pichani) katika kikao kazi cha Wajumbe wa Menejimenti na watumishi wa bodi hiyo, Mkoani Singida.
Baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti na Watumishi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RfB), wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Sekta ya Ujenzi, Ludovick Nduhiye, (hayupo Pichani), katika kikao kazi kilichofanyika Mkoani Singida.
Watumishi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wametakiwa kuzingatia miiko na utunzaji siri za Serikali pamoja na kuongeza ari ya utendaji kazi na utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi.
Akizungumza katika kikao cha Wajumbe wa Menejimenti na Watumishi wa Bodi ambacho kimefanyika mkoani Singida, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) Ludovick nduhiye, amesema utoaji siri za Serikali ni jambo la hatari ambalo linaweza kusababisha taharuki kwa jamii.
Ameongeza kuwa, kikao hicho pia kitasaidia kubadilishana uzoefu, kujenga mshikamano na kuchochea morali ya kazi kwa watumishi hivyo kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi wa bodi hiyo.
Baadhi ya Viongozi na Watumishi ambao wamehudhuria kikao hicho wameeleza umuhimu wa utunzaji siri na madhara ya kutofanya hivyo huku wakiwapongeza viongozi wa bodi hiyo kwa kuona haja ya kuwa na kikao kicho ambacho wanaamini kitakuwa mwarobaini wa kuondoa dosari zinazoweza kujitokeza katika utendaji kazi wa kila siku.