Na John Walter-Manyara
Suala la uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam kati ya serikali ya Tanzania na kampuni ya DP World Dubai bado linaendelea kugonga vichwa vya habari nchini Tanzania.
Kufuatilia hilo Chama cha Mapinduzi kanda ya Kaskazini ikijumuisha mikoa ya Arusha,Kilimanjaro na Manyara, kimeandaa mjadala maalum kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi juu ya suala hilo na umuhimu wake.
Mwenyekiti wa Chama chama Mapinduzi mkoa wa Manyara Peter Toima amesema watashiriki kikamilifu katika mjadala huo wa Jumamosi Julai 22,2023 wenye lengo la kuondoa mijadala iliyoenea katika mitandao ya kijamii na kusisitiza kuwa wanaosema Bandari itauzwa si kweli.
Toima amewataka Watanzania wasikubali kupotoshwa juu ya makubaliano yaliyofanywa na Tanzania na Dubai kuhusu uwekezaji bandari ya Daressalaam kwa sababu utakuwa na manufaa mengi kwa Taifa.
Amesema kiongozi katika mjadala huo utakaofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha atakuwa Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Daniel Chongolo.
Amesisitiza kuwa suala hilo lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020, na wao kama chama tawala wataendelea kuisimamia ilani inavyoelekeza.